Asilimia 50 ya watanzania kufikiwa na huduma za kibenki ifikapo 2025
Serikali imesema ili kufikia lengo hilo inaendelea na jitihada za kuweka mazingira mazuri ya kisera na kimifumo ili kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Posta Dkt. Edmund Mndolwa (kulia) wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Akaunti ya TABASAMU uliofanyika katika ukumbi wa Kisenga, jengo la LAPF jijini Dar es Salaam. Picha|Ofisi ya Makamu wa Rais.
- Serikali imesema ili kufikia lengo hilo inaendelea na jitihada kuweka mazingira mazuri ya kisera na kimifumo ili kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha nchini.
- Mama Samia amesema juhudi siende sambamba na kuwawezesha wanawake kupata huduma bora za kifedha ili kuinua shughuli za uzalishaji mali.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema itaendelea na jitihada kuweka mazingira mazuri ya kisera na kimifumo ili kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha nchini.
Mama Samia ambaye alikuwa akizungumza mara baada ya uzinduzi wa akaunti ya Tabasamu, iliyozinduliwa leo (Machi 28,2019) na Benki ya Posta Tanzania (TPB) jijini Dar es Salaam ambapo amesema mamlaka za Serikali zimeendelea kutoa miongozo ili kuhakikisha watanzania wanafikiwa kikamilifu na huduma za fedha katika maeneo yao ili kuchagiza shughuli za uchumi.
“Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutoa miongozo mbalimbali ili kuhakikisha watanzania takribani asilimia 50 wanafikiwa na huduma za kibenki ifikapo Mwaka 2025,” amesema Mama Samia.
Akizungumzia akaunti ya Tabasamu, amesema amependezwa na wazo la kuhakikisha kuwa kupitia akaunti hiyo, wanawake watauziwa bima za kijamii.
Benki ya Posta ina matawi takriban 80, mashine za kutolea pesa (ATM) 54, mtandao wa ‘Umoja Switch’ takriban 200 na mawakala 150 kupitia Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambapo Makamu wa Rais ameitaka benki hiyo kuwafikia wanawake wengi hasa wa vijijini na kuhakikisha wanapata huduma na elimu ya masuala ya kifedha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wanawake ni nguzo kuu ya uchumi, kwani wao ndiyo wazalishaji wakuu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
Soma zaidi:
- BOT yashusha riba tena kwa benki za biashara Tanzania.
- NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kijitali kwa mpigo
- Benki ya Mkombozi yapata bosi mpya
Mbali ya kulea familia, huwezi kuwakosa wanawake kwenye sekta yoyote ya uzalishaji mali, na hivyo siyo upendeleo kuanzisha akaunti maalumu ya Tabasamu kwa wanawake, bali ni haki yao ya msingi kama ilivyofanya benki ya TPB.
Makamu wa Rais ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji katika uzinduzi huo, ameitaka TPB kushirikiana na makampuni ya simu kuhakikisha kuwa wanawake si tu wanapata taarifa za kibenki hata ikiwezekana kuweza kupata huduma za kibenki kama mikopo kupitia simu zao za mikononi.
Naye Dk Kijaji amesema Tanzania ina rekodi nzuri Afrika na duniani kwa ujumla katika masuala ya huduma za kifedha.
Taasisi za fedha zimeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuongeza idadi ya wateja na kusogeza huduma karibu na watu ili kuhakikisha zinaendelea kubaki katika ushindani wa soko.