November 24, 2024

ATCL kuanza safari za China baada ya kuahirisha zaidi ya mara moja

Itaanza kufanya safari zake kuelekea jijini Guangzhou nchini China ifikapo Mei 8 mwaka huu baada kuahirishwa mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la Corona.

  • Imetangaza kuanza safari Mei 8 mwaka huu.
  • Safari hizo ziliahirishwa zaidi ya mara moja kutokana na Corona.
  • Safari hizo zitahusu watu maalum na mizigo. 

Dar es Salaam. Hatimaye Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaanza  kufanya safari zake kuelekea jijini Guangzhou nchini China ifikapo Mei 8 mwaka huu baada kuahirishwa mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la Corona. 

ATCL ilitarajia kuanza safari zake Machi 20 mwaka huu lakini zilisitishwa kutokana na hatua zilizowekwa na jiji la Guangzhou za kujikinga na COVID-19 ikiwa ni mara ya pili kuahirisha safari hiyo tangu Septemba mwaka jana. 

Hata hivyo, ATCL imetangaza tena kuanza kwa safari hizo za kuelekea China ifikapo Mei 8 mwaka huu kila siku ya Jumamosi na kurudi Jumapili. 

“Safari hizi zitakua mara moja kila baada ya wiki mbili,” imeeleza ATCL katika ukurasa wake wa Twitter. 

Hata hivyo, safari hizo ambazo zitakuwa zinatumia ndege aina ya Dreamliner zitakuwa kwa watu maalum wakiwemo raia wa China na mizigo.

“Kutokana na masharti yaliyowekwa na Serikali ya China, watakaoweza kusafiri kutoka Dar ni raia wa China na watu wenye vibali maalum, watakaoweza kusafiri kutoka China ni raia wa Tanzania pamoja na watu wengine,” imeeleza ATCL.


Soma zaidi: 


Shirika hilo ambalo kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/20 lilipata hasara ya Sh60 bilioni limesema hiyo ni fursa kwa Watanzania kusafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na China kwa gharama nafuu.

ATCL ni moja ya mashirika ya ndege Afrika Mashariki ambayo yamekua kwa kasi zaidi katika upanuzi wa idadi yake ya ndege na safari tangu Serikali ya hayati John Magufuli iingie madarakani mwaka 2015.

Ndani ya miaka mitano, ATCL iliongeza ndege nane na inatarajia kuwa na ndege 12 ifikapo 2021/22.

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake itaendelea kulilea Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kimkakati ili liweze kujiendesha kwa ufanisi ikiwemo kulitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi.