November 24, 2024

Azaki zapewa jukumu kuelimisha umuhimu wa kulipa kodi Tanzania

Wakati maonyesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) yakiendelea jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka Asasi hizo ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi ili zitumike katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka Asasi hizo ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
  • Amesema kodi hizo zitatumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 
  • Azitaka kutekeleza kikamilifu marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali namba 24 ya mwaka 2002.

Dar es Salaam. Wakati maonyesho ya Wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) yakiendelea jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka Asasi hizo ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi ili zitumike katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

Majaliwa alikuwa akizungumza jana jioni (Novemba 4, 2019) katika maonyesho hayo yanayofanyika uwanja wa Jamhuri ambapo yatafikia kilele chake Ijumaa, Novemba 8.

“Nitoe rai kwenu wana Azaki, muendelee kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili Serikali iweze kujenga miradi mikubwa ya kijamii,” amesema Majaliwa.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini kama vile kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo madiwani, viongozi wa vijiji na mitaa ili watambue majukumu yao.

“Niwatoe hofu tu kwamba Serikali inatambua mchango wenu wa kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo; kujiongezea kipato na kupata ujuzi; utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, afya, upatikanaji wa maji, huduma za kisheria na huduma za mikopo midogo.

“Pia tunatambua mchango wa Azaki wa kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi pale mnapoona kuna uhitaji. Pia mnaisaidia Serikali kupinga mila potofu na kandamizi hasa kwa makundi yenye mahitaji maalum,” amesema.


Zinazohusiana: 


Aidha, katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Azaki nchini zimetakiwa kuzingatia sheria iliyofanyiwa marekebisho ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali namba 24 ya mwaka 2002 na kanuni zake na kusisitiza kuwa marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta hiyo  na siyo kuyabana mashirika yasiyo ya kiserikali kama ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu.

Kuhusu mapato ya Azaki, Majaliwa amesema fedha wanazopata zinaweza kufanya miradi mikubwa ambayo itawanufaisha wananchi na akawasihi wazitumie kwenye ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana badala ya kuendesha semina na warsha.

“Tunajua fedha mnazopata zinaweza kusaidia kwenye miradi hii. Kwa mfano, kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, tulifanya mapitio ya ufadhili wa fedha mnazopata. Na katika upekuzi uliofanyika kwenye taasisi 92, ilibainika kwamba zilipokea jumla ya Sh261.059 bilioni 261. ambazo zimeingia kwenye Azaki hizi,” amesema Majaliwa katika taarifa hiyo. 

Azaki ni mkusanyiko wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakifanya kazi karibu na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali siyo rahisi kuzishughulikia zote na hivyo kuinua hali ya kiuchumi ya jamii husika. 

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mwaka huu, wizara yake imesajili mashirika yasiyo ya Kiserikali 617 ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017.

“Kati ya hayo mashirika 617, mashirika 44 ni ya ngazi ya kimataifa; 551 ni ngazi ya kitaifa, saba ni katika ngazi ya mikoa na mashirika 15 ni katika ngazi ya wilaya. Hadi kufikia Oktoba, 30, 2019, tumeshasajili mashirika 19,318,” amesema.