November 24, 2024

Bajeti wizara ya katiba yaongezeka baada ya kushuka miaka miwili

Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2021/22 imeongezeka hadi kufikia Sh78.5 bilioni baada ya kushuka mfululizo kwa miaka miwili iliyopita.

  • Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2021/22 imeongezeka hadi kufikia Sh78.5 bilioni.
  • Hii ni baada ya kushuka mfululizo kwa miaka miwili iliyopita. 
  • Fedha za maendeleo bado kitendawili katika wizara hiyo. 

Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2021/22 imeongezeka hadi kufikia Sh78.5 bilioni baada ya kushuka mfululizo kwa miaka miwili iliyopita. 

Waziri wa wizara hiyo Profesa Palamagamba Kabudi akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake bungeni jijini Dodoma leo amesema bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh73.6 bilioni zilizotengwa mwaka huu wa 2020/21.

Hata hivyo, Prof Kabudi amesema hadi Machi mwaka huu, wizara yake imepokea Sh46.8 bilioni sawa na asilimia 63.5 kati ya fedha zote zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2020/21. 

Katika kiasi cha fedha cha  Sh78.5 bilioni zinazoombwa kwa ajili mwaka 2021/22, Sh12.7 bilioni ni fedha za miradi ya maendeleo sawa asilimia 16.3 ya bajeti yote. Hii ina maana kuwa katika kila Sh100 zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo, Sh16 tu zimetengwa kwa ajili ya maendeleo.

Kupanda kwa bajeti ya wizara hiyo ambayo utekelezaji wake unaanza Julai mosi mwaka huu, huenda kukawapa kicheko wananchi ambao wanaitegemea wizara hiyo kwenye masuala muhimu ya kisheria, ikizingatiwa kuwa kwa miaka miwili mfululizo tangu mwaka 2019/20 bajeti ya wizara hiyo imekuwa ikishuka mfululizo. 

Licha ya kuwa bajeti ya mwaka 2021/22 imeongezeka hadi Sh78.5 bilioni haijaweza kufikia bajeti ya mwaka 2018/19 ambayo ilikuwa kubwa kuliko bajeti zote za wizara hiyo kwa miaka minne iliyopita.

Pia katika kipindi chote hicho bajeti inayoelekezwa katika miradi ya maendeleo haijawahi kuvuka robo ya bajeti yote, jambo ambalo linaibua maswali mengi kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya wizara hiyo kila mwaka.

Mathalan, mwaka 2019/20 miradi ya maendeleo ya wizara hiyo ilitengewa Sh30.1 bilioni na mwaka uliofuata ikashuka hadi Sh13.3 kabla haijaongezeka hadi Sh mwaka 2021/22.

Miradi itakayotekelezwa katika bajeti ya mwaka ujao ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa mahakama na kutafisri sheria zote za Tanzania na kanuni kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili ifikapo Desemba 2021. 

Hii itasaidia wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kuelewa kwa undani sheria mbalimbali na hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji haki katika mahakama za Tanzania.


Soma zaidi: 


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria Najma Giga ameishauri Serikali kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo zitolewe kwa wakati ili kuiwezesha kutimiza majukumu yake kama yalivyopangwa. 

“Serikali ihakikishe inatoa fedha hizo kwa wakati ili kuziwezesha taasisi (za Wizara ya Katiba na Sheria) hizo kupunguza changamoto za usafiri ikizingatiwa kuwa kazi nyingi zinafanyika nje ya ofisi na hivyo kuhitaji uhakika wa magari kumudu kazi zao na gharama nyinginezo za uendeshaji,” amesema Giga.

Pia kamati yake imeshauri wizara hiyo kuhakikisha utekelezaji wa vipaumbele vyake unaakisi udhibiti wa rasilimali za nchi, uharakishwaji wa utoaji haki, uboreshaji wa huduma za sheria, mazingira ya utoaji na upatikanaji haki kwa wakati.