Bajeti ya Serikali yaanza na maumivu kwa wamiliki vyombo vya moto
Kwa bei mpya za nishati za mafuta zilizotolewa na Ewura, Dar es Salaam ndio mkoa wenye ahueni.
- Ni baada ya kupanda kwa bei ya mafuta ya taa, petroli na dizeli.
- Sababu kuu ni utekelezaji wa bajeti mpya ya Serikali ya 2021/22.
- Kupanda kwa bei katika soko la dunia nako kwachangia.
Dar es Salaam. Wakati leo Julai 1, 2021, Serikali ikianza utekelezaji wa bajeti yake kwa mwaka 2021/22,watumiaji wa mafuta watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao baada ya nishati hiyo inayotumika kuendesha vyombo vya moto kupanda kwa viwango tofauti.
Kwa mujibu wa Bajeti Kuu ya Serikali iliyosomwa Juni 10 mwaka huu ilipendekeza kuwepo kwa tozo ya Sh100 kwa kila lita moja ya nishati ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, jambo lililochochea ongezeko la bei ikilinganishwa na mwezi Juni.
Kwa mujibu wa bei kikomo zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), petroli imepanda kwa asilimia 6.94 sawa na Sh156 kwa lita moja, dizeli (asilimia 6.87 sawa na Sh142) huku mafuta ya taa yakipanda kwa asilimia 8.38 sawa na Sh164.
Hiyo ni sawa na kusema wakazi wa Dar es Salaam wananunua lita moja ya petroli kwa Sh2,405, dizeli (Sh2,215) na mafuta ya taa kwa Sh2,121.
Bei za jumla za mafuta nazo zimepanda. Petroli inauzwa kwa Sh2,275, dizeli ikiwa ni Sh2,086 na mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh1,992.
Bei hizo ni kwa mafuta yanayopitia bandari ya Dar es Salaam.
Bei za mafuta zimekuwa zikipanda tangu mwanzoni mwa mwaka 2021. Picha. CitizenTV.
Maumivu hadi mkoani
Wakati nishati ya petroli na dizeli ikipanda bei, Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo wenye ahueni zaidi kwani kwa mikoa inayopokea mafuta katika bandari za Tanga na Mtwara, hali imebana zaidi.
Wakazi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambao mafuta yao yanapitia bandari ya Mtwara, wananunua petroli kwa Sh2,301 na Sh2,123 kwa dizeli kwa bei ya jumla.
Aidha, wale wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara ambao mafuta yao yanapitia bandari ya Tanga, bei ndiyo ipo juu zaidi kwani petroli inauzwa kwa Sh2,318 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,115 kwa bei za jumla.
“Mbali na mabadiliko katika kodi za mafuta na tozo za petroli, mabadiliko katika bei za ndani yamechangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia,” inasomeka taarifa ya Ewura iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje.
Bei ya petroli haishikiki
Huenda bei za mafuta zikaendelea kupanda katika miezi ijayo na kuwaumiza zaidi wamiliki wa vyombo vya moto kwa sababu bei hizo zimekuwa zikipanda mfululizo katika miezi ya hivi karibuni.
Mathalan, kuanzia mwezi Machi mwaka huu, petroli imekuwa ikiongezeka bei kwa zaidi ya Sh40 kila mwezi mkoani Dar es Salaam huku ongezeko la chini zaidi lilikuwa mwezi Mei ambapo bei ya petroli iliongezeka kwa Sh46 kutoka bei ya mwezi Aprili ya Sh2,123.