November 24, 2024

Balozi Mahiga azungumzia kompyuta zilizoibwa ofisi ya DPP

Siku mbili baada ya habari kusambaa nchini kuwa baadhi ya kompyuta katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) zimeibwa, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa wizi huo haukufanywa kwenye ofisi kuu na nyaraka za uhujumu anazoshug

  • Waziri wa Katiba na Sheria amesema wizi wa kompyuta ulioripotiwa siku za hivi karibuni ulitokea kwenye ofisi ndogo ya mkoa na siyo ofisi kuu ya DPP.
  • Amesema Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia mashtaka ya Serikali wala nyaraka za uhujumu uchumi hazikuguswa.
  • Amebainisha kuwa kitendo hicho cha uhalifu hakijaathiri hata kidogo uwezo wake na anaendelea na shughuli zake.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya habari kusambaa nchini kuwa baadhi ya kompyuta katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) zimeibwa, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa wizi huo haukufanywa kwenye ofisi kuu na nyaraka za uhujumu anazoshughulikia kiongozi huyo hazikuguswa.

Dk Mahiga amewaambia wanahabari leo (Oktoba 19, 2019) kuwa wizi huo ambao umeripotiwa katikati ya wiki uliofanyika katika ofisi ndogo ya mkoa wa Dar es Salaam ambapo anafahamu kuwa ni “vipande vya kompyuta mbili viliibwa” na siyo kompyuta zote.

“Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia mashtaka ya Serikali haikuguswa. Nyaraka zote zipo. Taarifa zote zipo na kazi yake inaendelea. Wizi huo ulitokea katika ofisi ndogo ya zamani ya Mkwepu, polisi wanaendelea na uchunguzi,” Mahiga amewaambia wanahabari baada ya kuulizwa undani wa wizi huo.

Jeshi la polisi lilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa lilipata taarifa za wizi huo Oktoba 15 na wanaendelea na uchunguzi.  


 Soma zaidi: 


Hadi jana ofisi ya DPP ilikuwa haijaweka bayana undani wa wizi huo ulioleta mjadala nchini hasa katika mitandao ya kijamii kutokana na kutokea katika kipindi ambacho DPP yupo katika majadiliano na baadhi ya watuhumiwa wa uhujumu uchumi ambao wamejitokeza kukiri makosa yao na kulipa fedha ili waachiwe.

Rais John Magufuli hivi karibuni alitoa fursa ya majadiliano baina ya DPP na watuhumiwa wa uhujumu uchumi ambao wapo tayari kukiri makosa yao, kutubu na kulipa waachiwe ili warudi uraiani kujumuika na familia zao na kuendeleza shughuli za maendeleo.  

“Nyaraka alizonazo DPP na anazozifanyia kazi hazijaguswa bado zipo. Kitendo hicho cha uhalifu hakijaathiri hata kidogo uwezo wake, zoezi lake na kumbukumbu tulizonazo kuhusu uhujumu uchumi,” amesema Dk Mahiga.

Amesema ofisi hiyo ndogo ya mkoa iliyopo Mtaa wa Mkwepu haishughulikii maagizo yoyote yanayohusu DPP bali ukusanyaji wa taarifa “fulani fulani.”