October 7, 2024

Barrick yatoa ahadi nyingine nne kwa Serikali ya Tanzania

Kampuni hiyo imewasilisha Sh231.43 bilioni kati ya Sh694.29 bilioni inayotakiwa kulipa ili kumaliza mgogoro wake na Serikali.

  • Ahadi hizo ni pamoja na kutoa Sh11.5 bilioni kwa ajili ya kuanza mchakato wa ujenzi wa mtambo wa kuchakata madini.
  • Pia Kampuni hiyo itaboresha kipande cha barabara ya Bulyanhulu na Mwanza pamoja na miundombinu mingine ili kunufaisha wakazi wa maeneo ya migodini.

Dar es Salaam. Licha ya kuwa kampuni ya madini ya Barrick Gold kukubali kuilipa Tanzania zaidi ya Sh684 bilioni ili kumaliza mgogoro wa kodi, pia imetoa ahadi nyingine nne kwa Serikali ikiwemo kutoa Sh11.5 bilioni kwa ajili ya kuanza mchakato wa ujenzi wa mtambo wa kuchakata madini nchini. 

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango aliyekuwa akizungumza leo (Mei 26, 2020) wakati akipokea sehemu ya malipo ya fidia kutoka Barrick Gold amesema ahadi zilizotolewa na kampuni hiyo zitasaidia kuwanufaisha Watanzania. 

Kampuni hiyo imewasilisha  Sh231.43 bilioni kati ya Sh694.29 bilioni inayotakiwa kulipa ili kumaliza mgogoro wake na Serikali.

Dk mpango amesema Barrick imekubali kutoa dola za Marekani 5 milioni (Sh11.5 bilioni) kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mtambo wa kuchaka madini nchini (Smelter).

Pia kampuni hiyo imekubali kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kutoa hadi dola za Marekani 10 milioni (Sh23.2 bilioni) kwa kipindi cha miaka 10 ambazo zinatarajiwa kusaidia utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini.

Pamoja na hayo, Barrick imekubali kutoa hadi dola za Marekani 6 (Sh13,885) kwa kila wakia ya madini itakayouzwa ambapo pesa hiyo itajumuishwa katika mfuko wa maendeleo ulioanzishwa na kampuni hiyo ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.

Waziri huyo amesema pia Barrick imekubali kutoa dola za Marekani 40 milioni (Sh92.5 bilioni) kwa ajili ya kuboresha kipande cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na miundombinu yake.

“Tunatumaini kwamba, pande zote mbili zinazohusika katika makubaliano zitaheshimu makubaliano na kuhakikisha yanatekekelezwa,” amesema Dk Mpango. 


Zinazohusiana


Wakati kampuni hiyo ikitoa ahadi hizo, Serikali tayari imeruhusu makontena ya makinikia ya dhahabu yaliyokuwa yamekwama bandarini kwa miaka mitatu yaanze kusafirishwa nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kumaliza mvutano na kampuni hiyo.

Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold (NYSE:GOLD) (TSX:ABX0) Mark Bristow katika taarifa yake iliyotolewa jana amesema matukio hayo ni sehemu za kuimarisha ushirikiano baina yake na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals iliyoanzishwa kwa ajili ya kusimamia rasilimali za madini za kampuni hiyo.

Katika kampuni hiyo ya Twiga Minerals, Barrick Gold inamiliki asilimia 84 wakati Serikali ikimiliki asilimia 16.