October 6, 2024

Barua yangu kwako miaka 10 ijayo

Kwa lolote unalofanya, tafadhali chukua kikombe cha maji na kisha vuta kiti uketi kwa kuwa ninayokuambia ni ya kutilia maanani.

  • Tafadhali, tenga muda kwa ajili ya wanaotenga muda kwa ajili yako iwe ni familia na jamaa wanaokuthamini.
  • Nakuomba anza kujijenga kwa kusoma na kujifunza.
  • Achana na tabia ya kubadilisha wenzi kila siku baki na mmoja atakayekujenga.

Kwako mzee baba. Sijafahamu ni nini unafanya wakati unafikiwa na barua hii. Huenda upo kitandani unaperuzi mtandaoni, upo mezani kwako ukifanyia kazi sanaa yako ama huenda upo kazini kwako ukiwa umefura kutokana na kukwaruzana na mhariri wako baada ya kukurudishia makala zako. Oooh, sina uhakika inawezekana ulishaacha uandishi. 

Kwa lolote unalofanya, tafadhali chukua kikombe cha maji na kisha vuta kiti uketi kwa kuwa ninayokuambia ni ya kutilia maanani.

Ni mwaka 2031 na sio jambo jema kukujuza kuwa mambo hayajawa kama ulivyokuwa umepanga. Kwa kuwa nimepata nafasi ya kukupatia ujumbe huu, huenda ikakusaidia kujirekebisha ili sehemu nilipo sasa, isiwe sehemu yako halisi mwaka huo ukifika.

Tafadhali rekebisha yafuatayo kwa ajili ya mustakabadhi mwema mzee baba.

Tumia muda wako vizuri

Unakumbuka ile tabia yako ya kuamka asubuhi unatumia dakika 30 kuwaza jinsi dunia inazunguka na kisha dakika 30 zingine kuperuzi kwenye mitandao na kuchati na wadau wako na zile dakika 10 unazozitumia kujivuta kutafuta bafu lilipo? Anza kuzitumia vizuri mshkaji wangu.

Tambua kuwa, kwa mahesabu rahisi, asubuhi nyingi huwa unapoteza saa zima ukiwa haujafanya chochote. Ni saa saba kwa wiki, saa 28 kwa mwezi na sawa na siku 14 (wiki mbili) kwa mwaka ukiwa unawaza dunia kuzunguka na kuchati mambo yasiyokujenga.

Badala ya kupoteza muda huo, anza kuutumia kwa kufanya mambo mazuri. Mfano, soma vitabu baadala ya kuchati, fanya mazoezi ya viungo na sauti, tumia muda mwingi na familia yako na uwapendao na pia, wahi kazini.

Afya yako ya baadaye ni matokeo ya unachokula na kukifanya leo. Picha| Nohat.

Tulia na mmoja mzee baba

Najua wewe ni kijana na damu inachemka hivyo huenda leo macho yapo kwa Irene, kesho yapo kwa Josephine na kesho kutwa kwa Salma lakini, unajua kuwa huenda ukichagua mmoja anayefaa kati ya wengi uwaonao atakusaidia kukujenga zaidi?

Ni mwaka 2031 na wanawake wapo tu tena wengi, wazuri mno hivyo kama unahisi utawamaliza wote, utakuwa unajidanganya mjomba. Pesa ambayo unaimaliza kwa kuwahudumia wote, itumie kumhudumia mmoja ambaye atakujenga.

Ningeliweza kukutajia jina la aliyepo sasa ambaye ameweza kukuvumilia. Ila huenda nikaharibu mambo kwa kuwa inaweza kukuangusha kwa ambaye siye japo wanaweza kuwa wamefanana majina.

Ni muda wako sasa kutulia na mmoja ambaye unamuona ana upeo mpana wa maisha, ana nia ya dhati na wewe na pia anakusaidia kuwa mwanaume bora kila kukicha. 

Yule ambaye hakukatii tamaa hata kama umejikatia tamaa mwenyewe. Unaweza sema namuelezea malaika lakini hata Waswahili wamesema, mchanga haufanani ukubwa. 


Soma zaidi:


Jifunze, jifunze, jifunze 

Nakujua tabia yako ya kusema “kama mtumbwi, unaenda na jinsi maisha yanavyokupeleka” lakini ni muda ukaachana nayo kwa kuwa upepo nao hubadilika na kama haujajipanga, utazama wewe na huo mtumbwi wako.

Ni muda sasa ukaacha kufanya mambo kwa mazoea kwa kuwa kuna ukuaji gani katika kufanya mambo ambayo unayajua kila siku? 

Tafadhali mzee baba, jifunze mambo mapya, chokoza batani ndani yako ambazo umezizima kwa uoga, hofu ya kushindwa na wasiwasi wa kutokufanya vizuri. 

Imba kama hautoimba tena, andika kana kwamba ni andiko lako la mwisho, shona nguo, tengeneza viatu, fanya biashara na fanya kila jambo kwa kuwa faida yake utaikuta huku hata kama hautoiona kwa hapo ulipo.

Kula vyema kwani afya yangu mwaka 2031 ni matokeo ya msosi wako Nakumbuka kuna wakati unaona shida kula chakula kizuri ulichopikiwa na shemeji yako. Badala yake unatoroka kidogo kwenda kula baga na viepe. Sio  mbaya ukifanya hayo mara moja moja lakini tafadhali usiendekeze.

Nimeongezeka kilo na sasa napata shida kuzipunguza lakini endapo utatilia maanani unachokula, kufanya mazoezi na kuijulia halli afya yako mara kwa mara huenda ukajiepusha na hali niliokuwa nayo. 

Rafiki zako ambao mlishibana pia hauna mawasiliano nao tena. Hauna mtu wa kupiga naye soga za miaka 10 iliyopita kwani wote ulio nao ni wapya. Picha| Larastock.

Tengeneza mahusiano mazuri

Najua wewe sio mtu rahisi kuongea na watu wapya mbele yako. Najua unapenda kukaa mwenyewe na kufurahia muda wako mwenyewe ukiamini ni salama na itakuepusha na watu wasiofaa katika mawasiliano yako.

Naomba nikuambie kuwa, rafiki zako ambao ni madaktari, hauna mawasiliano nao tena. Rafiki zako ambao ni wakurugenzi hauna mawasiliano nao tena. Rafiki zako ambao mlishibana pia hauna mawasiliano nao tena. Hauna mtu wa kupiga naye soga za miaka 10 iliyopita kwani wote ulio nao ni wapya.

Tafadhali, tenga muda kwa ajili yao sasa. Kutana nao pale unapopata muda. Sio mbaya mkatoka na kupata muda wa kukumbushiana jinsi ulikuwa mkorofi enzi za masomo yako na hata mara kadhaa ambazo uliwaomba chabo katika chumba cha mtihani.

Mpendwa, ni muda wa mimi kurudi katika majukumu yangu nikiwa na mawazo ya wapi nitapata fedha za kulipia ada kwa ajili ya watoto wako, wapi nitapata fedha za kulipia bili za nyumba na hata kuwasaidia wadogo zako. Tafadhali, tilia maanani niliyokuambia.

Wako katika wakati ujao, Rodgers George