November 24, 2024

Bei chanjo ya ugonjwa vichomi yashuka kwa asilimia 43

Itasaidia kuokoa maisha ya watoto katika nchini maskini ikiwemo Tanzania.

  • Bei hiyo ya dunia imeshuka kutoka Sh8,101 hadi Sh4,626.
  • Bei mpya itaanza kutumiaka Januari 2021. 
  • Itasaidia kuokoa maisha ya watoto katika nchini maskini ikiwemo Tanzania.

Dar es Salaam. Bei ya chanjo ya ugonjwa wa homa ya vichomi (nimonia) imeshuka kwa asilimia 43 na kufikia Dola za Marekani 2 kwa dozi moja na hivyo kuleta ahueni kwa nchi za kipato cha chini duniani ikiwemo Tanzania. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) katika taarifa yake iliyotolewa katika miji ya New York, Marekani na Geneva, Uswisi imesema kuwa punguzo hilo linafuatia makubaliano mapya kati ya UNICEF na taasisi ya Serum ya India (SII).

Bei mpya ya dola 2 (Sh4,626) imepungua kwa asilimia 43 kutokana makubaliano ya awali ya chombo kinachosimamia soko la chanjo hiyo (AMC) na mfuko wa chanzo duniani (GAVI)  iliyokuwa dola za Marekani 3.50 (Sh8,101) ambayo matumizi yake yanakamilika Desemba mwaka huu. 

Bei hiyo mpya itasaidia kuondoa uhaba wa chanjo na kuokoa maisha ya watoto katika nchi maskini ambako ugonjwa wa homa ya vichomi ni moja ya sababu kubwa ya vifo.

“Makubaliano haya ya usambazaji na bei ni ya nane kufanyika na ya kwanza kujumuisha kampuni ya kutengeneza dawa kutoka nchi inayoendelea. 

“Kwa mujibu wa mkataba, kampuni ya dawa ya India itayapatia mataifa yanayopata msaada kutoka GAVI, dozi milioni 10 za chanjo dhidi ya homa ya vichomi kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10 ijayo,” imesema taarifa ya UNICEF.


Soma zaidi: Chanjo ya virusi vya Corona yaanza kufanyiwa majaribio


UNICEF imesema bila makubaliano kama hayo, chanjo ya nimonia inaweza kuzifikia nchi maskini ambazo zina mzigo zaidi wa ugonjwa huo kati ya miaka 10 hadi 15 tangu kutengenezwa kwake.   

Chini ya AMC, chanjo hiyo ya vichomi imefikia zaidi ya nchi 60 za kipato cha chini ambako kiwango cha utoaji wa chanjo hiyo ni asilimia 48, kiwango ambacho ni cha juu kuliko kile cha wastani cha asilimia 47 duniani kote.

Mkurugenzi wa UNICEF anayehusika na usambazaji na manunuzi Etleva Kadili amesema nimonia ni muuaji mkubwa wa watoto, inasababisha kifo cha mtoto mmoja kila katika sekunde 39.

“Kwa kuweza kupeleka chanjo hiyo kwa bei nafuu, tunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto. Mfumo wetu bunifu umewapatia motisha wazalishaji kutuletea chanjo hii kwa uwezo wa soko,” amesema Kadili.