Bei ya chakula duniani yapanda kwa miezi saba mfululizo
Kupanda kwa bei hizo kunatoa tafsiri mbalimbali ikiwemo kuwafaidisha wakulima na kuwafanya wanunuzi kutoboa mifuko yao zaidi ili kuzipata bidhaa hizo.
- FAO imetangaza kupanda kwa bei za vyakula kwa miezi saba mfululizo kufikia Desemba 2020.
- Kati ya vyakula vilivyopanda bei ni mahindi, ngano na mafuta ya mbogamboga.
Dar es Salaam. Bei ya vyakula duniani imepanda kwa miezi saba mfululizo hadi kufikia Desemba, 2020 ikichagizwa na bidhaa za maziwa na mafuta ya mbogamboga.
Kupanda kwa bei hizo kunatoa tafsiri mbalimbali ikiwemo kuwafaidisha wakulima na kuwafanya wanunuzi kutoboa mifuko yao zaidi ili kuzipata bidhaa hizo.
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) katika taarifa yake ya Desemba 7, 2020, limesema ongezeko la bei hizo limekua kwa asilimia 2.2 mwezi Desemba 2020 hadi kufikia pointi 107.2 kutoka pointi 105.2 iliyorekodiwa mwezi Novemba.
Bei za vyakula duniani zimekuwa zikipanda mfululizo tangu mwezi Juni mwaka jana.
Kwa mujibu wa FAO, bei ya kuuza nje vyakula ikiwemo ngano, mahindi, mtama na mchele ilipanda kwa sababu ya wasiwasi juu ya hali ya ukuaji na matarajio ya mazao hasa kaskazini na kusini mwa Marekani pamoja na Urusi.
Soma zaidi:
- Ahueni, maumivu: Bei mpya za petroli, dizeli Tanzania
- Mfumuko wa bei washuka baada ya ‘kuganda’ kwa miezi miwili Tanzania
- Serikali yaeleza sababu kupungua usafirishaji mizigo uwanja wa ndege Mwanza
FAO inaeleza kuwa, kwa mwaka 2020 bei za kuuza nje mchele zilikuwa asilimia 8.6 juu kuliko mwaka 2019, wakati zile za mahindi na ngano zilikuwa asilimia 7.6 na asilimia 5.6 juu, mtawaliwa.
Bei ya mafuta ya mbogamboga iliongezeka kwa asilimia 4.7 mnamo Desemba mwaka jana kufikia kiwango cha juu kabisa tangu Septemba 2012.
Kwa upande wa bidhaa za maziwa, FAO inaonyesha bei zilipanda kwa asilimia 3.2 mwezi Desemba 2020 ikiwa ni ongezeko mfululizo kwa miezi saba.
Kwa nyama, bei ziliongezeka kwa asilimia 1.7 ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo kiwango cha juu cha bei kilipanda kwa asilimia 4.5.
Hata hivyo, kiwango cha bei ya sukari kwa mujibu wa FAO kilipungua kwa asilimia 0.6 mnamo Desemba mwaka jana baada ya ongezeko kubwa wakati wa mwezi Novemba. Kwa mwaka 2020 kwa ujumla, ongezeko lilikuwa asilimia 1.1 juu kuliko mwaka 2019.