July 8, 2024

Bei ya mahindi yaporomoka kwa kasi Dodoma

Bei ya jumla ya mahindi katika Mkoa wa Dodoma imeshuka kwa takriban asilimia 44 ndani ya kipindi cha wiki moja, jambo linawapa ahueni wanunuzi wa zao hilo katika mkoa huo uliopo katikati mwa Tanzania.

  • Bei ya juu ya zao hilo kwa kilo 100 mkoani humo imeshuka hadi Sh50,000 kutoka Sh90,000 Jumatatu iliyopita.
  • Lindi ndiyo mkoa ambao mahindi yanauzwa kwa bei ya juu zaidi Tanzania.

Dar es Salaam. Bei ya jumla ya mahindi katika Mkoa wa Dodoma imeshuka kwa takriban asilimia 44 ndani ya kipindi cha wiki moja, jambo linawapa ahueni wanunuzi wa zao hilo katika mkoa huo uliopo katikati mwa Tanzania. 

Takwimu za mazao makuu ya chakula zilizotolewa leo (Aprili 27, 2020) na Wizara ya Viwanda na Biashara zinaonyesha kuwa bei ya juu ya gunia la kilo 100 la zao hilo humo linauzwa kwa Sh51,000 katika soko la Kibaigwa.

Hata hivyo, bei hiyo ya juu imeshuka kwa asilimia 43.3 kutoka Sh90,000 iliyorekodiwa Jumatatu Aprili 20, 2020 mkoani humo katika soko la Majengo. Katika takwimu za leo, bei ya juu ya zao hilo katika soko hilo la Majengo imeporomoka hadi Sh50,000 huku ya chini ikiwa ni Sh45,000 chini ya ile iliyorekodiwa wiki moja iliyopita ya Sh60,000.   

Kushuka kwa bei hiyo ya juu kutawanufaisha zaidi wanunuzi huku wafanyabiashara na wakulima wakipoteza wastani wa Sh39,000 kwa kila gunia moja iwapo hesabu hizo zitapigwa kwa viwango vya bei ya juu. 

Bei hiyo iliyotumika wiki iliyopita mkoani Dodoma ndiyo ilikuwa bei ya juu ya zao hilo Tanzania Bara kwa mujibu wa takwimu hizo za wizara. 


Soma zaidi: 


Wakati bei ya juu mkoani humo ikishuka, pia bei ya chini imeshuka hadi Sh45,000 kutoka Sh49,000 iliyorekodiwa wiki iliyopita. 

 Aidha, takwimu hizo zinaonyesha kuwa bei ya zao hilo la chakula inayotumika leo ni Sh120,000 katika Mkoa wa Lindi huku bei ya chini ikiwa ni Sh30,000 katika Mkoa wa Ruvuma. 

Endelea kusoma www.nukta.co.tz kwa kwa habari zaidi za takwimu kuhusu bei za mazao, soko la hisa na nyingine za biashara. Kwa habari zaidi Whatsapp +255 677 088 088 au newsroom@nukta.co.tz