Bei ya pembejeo yawakera wakulima Njombe
Baadhi ya wakulima wa Halmashauri ya mji wa Njombe wamesema hawana uhakika kama watafaidika na shughuli za kilimo msimu huu kutokana na kupanda kwa bei za pembejeo ikiwemo mbolea.
- Wasema bei ya mbolea imepanda kinyume na matarajio yao.
- Hawana uhakika kufaidika na kilimo msimu ujao.
- Serikali yasema inashughulikia suala la bei ya mbolea.
Njombe. Baadhi ya wakulima wa Halmashauri ya mji wa Njombe wamesema hawana uhakika kama watafaidika na shughuli za kilimo msimu huu kutokana na kupanda kwa bei za pembejeo ikiwemo mbolea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini na wananchi, wakulima hao wamesema kwa sasa bei za mbolea zinaanzia Sh85,000 hadi Sh100,000 kwa mfuko mmoja bei ambayo wamedai kuwa inawaingizia hasara katika kilimo chao.
Wamedai gharama za uzalishaji haziendani na bei ya mazao wanayouza sokoni kwa sababu ziko chini na hivyo kuwaingizia hasara.
Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika amesema kupanda kwa bei za pembejeo siyo mpango wa Serikali kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani, bali ni kutokana na uhaba wa mbolea katika nchi zinazozalisha kwani asilimia kubwa ya mbolea zinazotumika nchini hutoka nje.
Amewataka wananchi kuwa wavumilivu kwani Serikali inalishughulikia suala hilo kwa haraka zaidi na kabla ya msimu wa kilimo haujanza huenda litakua limeshughulikiwa.
Mwanyika anaendelea na ziara za kukutana na wananchi na mpaka sasa ameshafanya ziara katika kata za Matola na Makowo na Julai 23,2021 anatarajiwa kufanya ziara katika kata ya Luponde.
Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ili kuhakikisha changamoto za mbolea zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini badala ya vibali hivyo kutolewa na Waziri.
Prof Mkenda amesema kwa sasa uingizaji wa mbolea umeongezeka hapa nchini na wakulima wataanza kuipata katika maeneo yao.
“Hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini wanaohifadhi mbolea wakidhani bei itapanda, hilo hapana itashuka hivyo ni bora kuiuza mbolea hiyo mapema,” amesema Waziri huyo leo Julai 20, 2021.