November 24, 2024

Bei za mafuta zapanda duniani baada ya kifo cha Jenerali wa Iran

Bei za mafuta zimepanda kwa zaidi ya asilimia tatu kwenye soko la dunia baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran, Jenerali Qasem Soleimani.

  • Bei za mafuta zimepanda kwa zaidi ya asilimia tatu kwenye soko la dunia baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran, Jenerali Qasem Soleimani.
  • Tukio hilo pia lilisababisha mtikisiko kwenye masoko ya hisa dunia na biashara za makampuni ya mafuta. 
  • Aliuawawa jana na anazikwa leo nchini Iraq.

Bei za mafuta zimepanda kwa zaidi ya asilimia tatu kwenye soko la dunia baada ya Marekani kumuua kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran, Jenerali Qasem Soleimani, kisa kilichozusha hofu ya kuibuka mzozo Mashariki ya Kati iliyo na utajiri mkubwa wa nishati hiyo. 

Kwa mujibu wa duru za kimataifa, pipa moja la mafuta ghafi katika soko hilo limefikia dola za Marekani 69.50 sawa na Sh159,827, kiwango ambacho ni cha juu zaidi tangu Septemba 2019 ambapo ilikuwa dola 68.

Soleimani, alilengwa na kuuawa nje ya uwanja wa ndege wa Baghdad, katika shambulio la anga ambalo liamriwa na Rais wa Merekani, Donald Trump, kulingana na taarifa iliyotolewa na Idara ya Ulinzi ya Marekani.

Kiongozi wa wanamgambo wa Iraq,  Abu Mahdi al-Muhandis, alikuwa pia miongoni mwa wale waliouawa wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

Tukio hilo pia lilisababisha mtikisiko kwenye masoko ya hisa duniani na biashara za makampuni yanayohusika na uuzaji wa mafuta ya petroli na dizeli katika shughuli mbalimbali za uzalishaji. 

Kwa mujibu wa duru za Habari, Kiongozi mkuu wa Iran, Ayattollah Ali Khamenei, ametoa taarifa akitaka siku tatu za maombolezo ya umma kufuatia kifo cha Jenerali Soleimani na kusema kuwa watalipa kisasi dhidi ya mashambulizi hayo ya Marekani.

Hata hivyo, maafisa wa wizara ya ulinzi wa Pentagon, wamesema Marekani itapeleka wanajeshi 3000 wa ziada kwenye eneo la mashariki ya kati kukabiliana na kitisho kinachoongezeka.

Muombolezaji akiwa ameshika picha ya Qasem Soleimani ambaye mazishi yake yanafanyika leo baada ya kuawawa nchini Iraq. Picha|Mtandao.

UN yaingilia kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guaterres ameelezea wasiwasi wake na kutoa wito wa kupunguza mvutano katika eneo lote la Ghuba (Mashariki ya Kati)  baada ya kuuawa kwa Jenerali Soleimani.

Guterres katika taarifa yake iliyotolewa jana asubuhi na  msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema kuwa mkuu huyo wa UN alikuwa anatetea mara kwa mara akichagiza kupunguza mvutano na kuongeza kuwa huu ni wakati ambao viongozi lazima watulie zaidi na kujizuia na machafuko.

“Huu ni wakati ambao viongozi wanapaswa kujizuia na mvutano Zaidi. dunia haiwezi kumudu vita vingine Ghuba,” amesema Guaterres katika taarifa hiyo.


Zinazohusiana: 


Jenerali Soleimani alikuwa mtu mashuhuri kwa utawala wa Iran. Kikosi chake cha Qudsi kinachofanya kazi katika nchi za kigeni kilikuwa kinaripoti moja kwa moja kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Khamenei na alisifiwa kama shujaa wa kitaifa.

Kifo cha afisa huyo, kinakuja baada ya siku kadhaa za maandamano ambapo waandamaanaji waliokuwa wakishambulia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, Iraq kukabiliana na vikosi vya Marekani katika eneo hilo.

Pentagon inasema jenerali Soleimani aliidhinisha mashambulio dhidi ya ubalozi.

Mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji na mauaji ya kupangwa, Agnes Callamard amehoji uhalali wa mashambulio hayo ya anga ya Marekani chini ya sheria za kimataifa na kuutaka Umoja wa Mataifa kutumia jukwaa na nyezo za kisheria ilizonazo kuingilia kati suala hilo. 

“Hakuna wakati mwingine wowote wa muhimu na wa shinikizo kwa Umoja wa Mataifa na uongozi wake kama sasa,” ameandika Callamard.