November 24, 2024

Benki ya Dunia yabadilisha maamuzi wafanyakazi wake kutembelea Tanzania

Benki hiyo sasa imeondoa zuio la wafanyakazi wake kuzuru nchini lililokuwa limewekwa hapo awali kwa madai ya “kuwepo vitisho na ubaguzi dhidi ya watu wanaotekeleza vitendo vya ushoga”.

  • Benki hiyo sasa imeondoa zuio la wafanyakazi wake kuzuru nchini lililokuwa limewekwa hapo awali kwa madai ya “kuwepo vitisho na ubaguzi dhidi ya watu wanaotekeleza vitendo vya ushoga”.

Dar es Salaam.  Siku sita tangu Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia  Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem azuru nchini na kufanya mkutano na Rais John Magufuli Ikulu (Novemba 16,2018), benki hiyo imeondoa zuio la wafanyakazi wake kutembelea Tanzania lililokuwa limewekwa kutokana na sababu ilizodai ni “uvunjifu wa haki za binadamu ukiwemo ubaguzi dhidi wapenzi wa jinsia moja.”

Ghenem alikuwepo Tanzania juma lililopita ambapo pamoja na mengine walijadiliana na Serikali kuhusu mkopo wa Dola za Marekani 300 Milioni (zaidi ya Sh680 bilioni kwa ajili ya mradi wa kuboresha elimu ya sekondari nchini. 

Awali benki hiyo haikuwasilisha mkopo huo kwa Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya kuupitisha kutokana na kutoridhishwa na hatua ya Serikali kuzuia wanafunzi wajawazito kutoendelea na masomo katika shule za umma. 


Zinazohusiana:


Taarifa iliyotolewa na benki hiyo Novemba 20,2018 imeeleza kuwa uamuzi wa kuondoa zuio hilo umekuja baada ya Serikali kuihakikishia benki hiyo kuwa Tanzania haitatekeleza hatua yoyote ya “ubaguzi, unyanyasaji, kukamatwa kwa watu binafsi kutokana na mwelekeo wao wa kijinsia.”

Benki hiyo imetaka mazingira jumuishi katika jamiii  bila ubaguzi wa kiumri, jinsia, kabila, dini, kimwili, akili au ulemavu mwingine, hali ya afya, mwelekeo wa kijinsia, utambulisho wa kijinsia, urithi wa asili na hali ya kiuchumi.

“Baada ya kuhakikishiwa na mamlaka za Tanzania na kufuatia tathimini ya usalama ya ndani, uongozi wa  Benki ya Dunia, kwa kushauriana na wafanyakazi wake nchini na washirika wengine wa maendeleo, imeamua kuondoa katazo la kutembelea Tanzania. Wakati huo huo inafuatilia kwa karibu ili kupima hali iliyopo na kuchukua hatua zinazofaa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Benki ya Dunia.