November 24, 2024

Benki ya Dunia yaeleza sababu za kuipatia Tanzania mkopo wa Sh1 trilioni

Yasema imeridhishwa na utekelezaji wa mpango wa kipindi cha pili wa kunusuru kaya masikini ambao upo chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

  • Yasema imeridhishwa na utekelezaji wa mpango wa kipindi cha pili wa kunusuru kaya masikini ambao upo chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
  • Mkopo huo wa masharti nafuu umelenga kutekeleza awamu ya tatu ya mpango wa TASAF wa kupunguza umaskini kwa Watanzania. 
  • Mkopo huo utasaidia kuboresha elimu, kuwainua Watanzania kiuchumi na kuwapatia kipato cha kaya. 

Dar es Salaam. Benki ya Dunia imeipatia Tanzania mkopo wa Sh1.03 trilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kipindi cha pili wa kunusuru kaya masikini ambao upo chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya tatu.

Kutolewa kwa mkopo huo wa masharti nafuu ni matokeo ya kufanikiwa kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Tasaf kati ya mwaka 2000 na 2005 uligharibu Sh72 bilioni. 

Fedha hizo zilitumika katika miradi ya kijamii takriban 1,704 ya kujenga madarasa, barabara, vituo vya afya, miradi ya umwagiliaji na mabwawa ya kuhifadhia maji kwa ajili ya kaya maskini. 

Katika awamu ya pili (2005-2013), Tasaf  ilitekeleza miradi ya kijamii 12,347 yenye thamani ya Sh430 bilioni na kuwanufaisha watu milioni 18.6.

Makubaliano ya kuipatia Tanzania mkopo huo, yamefanyika  kati ya  ya Katibu Mkuu wa Hazina, Doto James na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Bella Bird jana (Oktoba 7, 2019) jijini Dar es Salaam.

Mkopo huo wa masharti nafuu ulioidhinishwa na Bodi ya Benki ya Dunia Septemba 12 mwaka huu, unasaka kuimarisha lishe bora na kuinua kipato huku ukiongeza mahudhurio ya watoto katika shule za msingi kuwawezesha kumaliza masomo, sambamba na kupata huduma za afya.

Mwakilishi huyo wa Benki  ya Dunia akizungumza baada ya utiaji saini amenukuu takwimu za tathmini  ya kati ya mradi huo amebainisha kuwa, 

“TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika kufikia wale walio maskini zaidi nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 60 ya wanufaika wa mradi huu wako kwenye kundi la asilimia 20 ya watu maskini zaidi kwa vigezo vya matumizi.”

Amesema kuwa kaya zinazopokea fedha kupitia mradi huo wa kunusuru kaya maskini zimepunguza umaskini kwa asilimia 10 na kuongeza kwa asilimia 20 kiwango chao cha matumizi kwa mwezi ikilinganishwa na kaya ambazo hazikupata msaada huo.

Mabadiliko yameonekana pia kwenye idadi ya watoto wanaoandikishwa shuleni, kiwango cha kujua kusoma na kuandika, wanawake kufika katika huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za afya kwa mtoto.

Pia bila kusahau bima ya afya, uhakika wa kupata chakula na umiliki wa mali,  jambo ambalo amesema ni muhimu katika kutokomeza umaskini.


Zinazohuziana


Kupitia mkopo huo, James amesema miradi ambayo inatoa ajira za muda mfupi hasa zenye kuhusisha ujenzi wa miundombinu kwenye sekta mahususi zikiwemo afya, elimu na maji itatekelezwa. 

Pia, amesema kuwa uimarishaji wa taasisi na mifumo hautaachwa nyuma katika mradi huo. 

Utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na  Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (FYDP 2016 – 2021)., Mkakati wa Kukuza Uchumi na  Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) utakaoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema James.

Endapo mradi huo utafanikiwa, kaya hizo zitaweza kukuza uchumi wake na kujenga rasilimali watu hasa watoto wanaohudhuria kliniki na wale walioko shuleni na wenye kuishi kwenye mazingira magumu.

Mabadiliko yameonekana pia kwenye idadi ya watoto wanaoandikishwa shuleni, kiwango cha kujua kusoma na kuandika, wanawake kufika katika huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na huduma za afya kwa mtoto. Picha|Mtandao.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tasaf, Dk Moses Kusiluka, amezihimiza kaya masikini kutumia fursa hiyo kwa kuongeza kipato na huduma za jamii huku lengo kuu likiwa ni kupunguza umasikini uliokithiri.

Dk Moses amesema anaamini kupitia fedha hizo jamii itanufaika huku akitoa ahadi ya kuzisimamia kikamilifu fedha zinazotolewa ili zitumike kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shaaban Mohamed, amesema Zanzinbar imekuwa mnufaikaji mkubwa wa mpango huo wa kunusuru kaya maskini.

“Mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote mbili imepelekea Serikali kutekeleza awamu ya tatu (TASAF III) mwaka 2012, ambayo itatekelezwa kwa miaka 10 mpaka 2023 katika vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza kitafikia ukomo mwaka huu 2019, na Awamu ya Pili ambayo mkataba wa mkopo umesainiwa, utakamilika mwaka mwaka 2023,” amesma Mohamed.

Serikali ilianzisha mfuko wa Tasaf mwaka 2000 huku dhumuni kuu likiwa ni kupunguza kuinua maisha ya kaya maskini Tanzania.