November 24, 2024

Benki ya Dunia yaiwekea vikwazo kampuni iliyojenga vituo vya biashara ya mipakani Tanzania

Ni kampuni ya SAI ya nchini India inayodaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa wakati wa ujenzi miradi mitatu barani Afrika ikiwemo vituo vya pamoja vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

  • Ni kampuni ya SAI ya nchini India iliyojenga miradi mitatu barani Afrika.
  • Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya pamoja vya mipakani vya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2015. 
  • Vikwazo hivyo vitaizuia SAI kushiriki miradi ya Benki ya Dunia kwa miaka miwili isipokua kwa masharti maalum.

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeiwekea vikwazo kampuni ya SAI Cunsulting Engineering Ltd (SAI) ya India kwa miaka miwili  ikituhumiwa kwa vitendo vya rushwa katika ujenzi wa miradi mitatu barani  Afrika ikiwemo ujenzi wa vituo vya pamoja vya mipakani nchini Tanzania. 

Miradi hiyo inayodaiwa kugubikwa na rushwa ni pamoja na mradi wa Afrika Mashariki wa kuimarisha biashara na usafiri; mradi wa Msumbiji wa usimamizi na ukarabati wa barabara na madaraja; na mradi wa Ghana wa sekta ya usafirishaji.

Taarifa iliyotolewa na benki hiyo jana (Julai 10, 2019) jijini Washington, Marekani inaeleza kuwa vikwazo ilivyowekewa SAI ni kwa sababu ilikiuka masharti ya mkataba na itaruhusiwa kushiriki miradi ya benki hiyo kwa masharti maalum. 

Inadaiwa kuwa SAI ilikuwa inatoa fedha taslimu za vocha na zawadi kwa maafisa wa mradi wa ujenzi wa vituo vya pamoja vya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukwepa malipo halali yaliyoidhinishwa kwenye mkataba. 

Mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulibuniwa kuboresha mazingira ya biashara na usafirishaji katika Umoja wa Forodha wa jumuiya hiyo kwa kujenga vituo vya pamoja mipakani ambao ulikamilika mwaka 2015. 

Kwa mujibu wa benki hiyo, SAI imekubali kuwajibika kwa vitendo vya rushwa vilivyotokea wakati wa utekelezaji wa miradi yote mitatu na kama haitawajibika itazuiwa kushiriki katika miradi yote inayofadhiliwa na benki hiyo. 


Zinazohusiana:


Vituo vya pamoja vya Tanzania vimejengwa katika mipaka ya Kabanga, Rusumo na Mtukula vya mkoani Kagera vinavyopakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi. 

Vituo hivyo vimekuwa kiunganishi muhimu cha shughuli za biashara na uhamiaji katika mipaka ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambavyo vinarahisisha mzunguko wa pesa na muingiliano wa watu katika ukanda huo. 

Benki ya Dunia katika taarifa yake, imeeleza kuwa kama ilivyo kwa mradi wa vituo vya pamoja, SAI pia ilikuwa inatoa malipo ya pesa taslimu kwa wasimamizi wa miradi ya Ghana na Msumbiji ambapo ni kinyume na makubaliano ya mkataba. 

Makubaliano ya kuiwekea kampuni hiyo vikwazo yalifikiwa na Benki ya Dunia na kampuni ya kimataifa ya uhandishi ya  SYSTRA ya Ufaransa ambayo inamiliki asilimia 65 ya hisa za SAI. 

Hata hivyo, vikwazo hivyo vilipunguzwa baada ya SYSTRA kuripoti kwa Benki ya Dunia kuhusu vitendo vya rushwa vilivyofanywa na SAI katika miradi hiyo.