Benki ya Mkombozi yapata mkurugenzi mpya
Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya biashara ya Mkombozi imteua Respige Kimati kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya kuanzia Januari 18, 2020, huku akiwa na kibarua cha kuboresha mfumo wa uendeshaji wa benki hiyo.
- Ni kigogo aliyewahi kufanya kazi katika benki za Standard Charted, Stanbic na KCB.
- Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na George Shumbusho. aliyehudumu tangu mwaka 2017.
Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya biashara ya Mkombozi imteua Respige Kimati kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya kuanzia Januari 18, 2020, huku akiwa na kibarua cha kuboresha mfumo wa uendeshaji wa benki hiyo.
Kimati ambaye ni moja ya watu maarufu katika sekta hiyo ya fedha, anachukua nafasi ya iliyoachwa wazi na George Shumbusho aliyehudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2017.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Menejimenti ya Bodi ya benki hiyo katika vyombo vya habari leo, Februari 24, 2020 imeeleza kuwa Kimati ana uzoefu wa miaka 11 ya kushika nafasi za juu za uongozi katika taasisi za fedha na hivyo inaamini mchango wake utasaidia katika ukuaji wa benki hiyo iliyooanzishwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) mwaka 2009.
“Uzoefu wake wa kitaaluma unamuweka katika nafasi ya kutoa mchango wake muhimu wa kimkakati katika ukuaji endelevu na biashara yenye faida katika sekta ya fedha,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi Profesa Marcellina Chijoriga.
Kabla ya uteuzi huo mpya katika benki hiyo inayotoa huduma za mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, Kimati aliwahi kuzitumikia benki kubwa nchini zikiwemo Standard Charted,Stanbic, KCB, Ecobank na kampuni ya Capital Finance Limited.
Kimati mwenye shahada ya uzamili ya Fedha (MSc) kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde cha nchini Uingereza, ni mtaalamu wa uuandaji na tathmini ya miradi, uchambuzi wa mikopo na usimamizi wa shughuli za mahusiano ya kibenki.
Soma zaidi:
Kibarua alichonacho Kimati
Kimati atakuwa na kibarua kigumu cha kuongoza timu yake katika utekelezaji wa mpango wa benki wa mwaka 2019 hadi 2021 ambao unalenga kubadilisha mfumo wa uendeshaji shughuli za benki kutoka uwekezaji wa rasilimali nyingi katika uendeshaji na kwenda kwenye mfumo utakaoweka mkazo na uwekezaji wa rasilimali zaidi katika uuzaji na utoaji huduma na bidhaa za kibenki.
“Hili litahusisha mabadiliko mengi ikiwemo kubadilisha mifumo ya ndani ya utoaji huduma pamoja na mitiririko yake na kuziweka shughuli zote za kibenki katika eneo moja kiutendaji,” inaeleza sehemu ya mpango huo.
Pia kubadilisha mizania ya hesabu za benki kimuundo (fedha za kitanzania dhidi ya fedha za Kigeni), kuoanisha vyanzo vya faida ya benki na malengo ya mapato ya benki katika mwaka pamoja na kuweka vyema mizania bora, vyanzo vya mapato yasiyotokana na mikopo na uwekezaji kwa kuanzisha huduma saidizi za biashara.
Katika kipindi cha miaka mitatu, benki hiyo inalenga kuwezesha mifumo ya malipo na ukusanyaji ili kurahisisha shughuli za kibenki (kwenda kidijitali zaidi).
Mkombozi Bank ni moja ya benki muhimu kwa ukuzaji wa biashara nchini kutokana na kutoa huduma za mikopo ya vikundi, kilimo, biashara, vifaa na uwekezaji na mikopo inayotokana na dhamana ya mishahara.