Benki za Tanzania zaanza kuondoa tozo za miamala ya simu
Benki za biashara za Tanzania zimeanza kuondoa tozo za miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya simu (simu benki) ikiwa ni hatua ya kuwapunguzia wananchi makali ya athari ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
- Ni miamala inayofanyika kwa njia simu za mkononi ili kuwapunguzia makali wananchi kukabiliana na Corona.
- Benki ya Access imeondoa tozo zote kuhamisha fedha chini ya Sh200,000.
- Kampuni za bia nazo zaombwa kuzalisha vitakasa mikono ili kuwapatia wananchi ahueni.
Dar es Salaam. Benki za biashara za Tanzania zimeanza kuondoa tozo za miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya simu (simu benki) ikiwa ni hatua ya kuwapunguzia wananchi makali ya athari ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
Hatua hiyo inakuja baada ya aliyewakuwa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba kuzishauri benki na kampuni za simu nchini kuondoa tozo ya miamala inayofanyika kielektroniki isiyozidi Sh50,000.
Makamba alitoa ushauri huo katika ukurasa wake wa Twitter Machi 19, 2020 huku akibainisha kuwa itahamasisha wananchi wengi kutumia njia mbadala za simu benki kipindi hiki cha mlipuko wa Corona duniani.
Benki ya Access imekuwa ya kwanza kuupokea ushauri huo wa Makamba na kuondoa tozo katika huduma ya kutuma pesa kwa miamala iliyo chini ya Sh200,000.
“Tunashukuru kwa ushauri @JMakamba , tumeufanyia kazi na tunapenda kukufahamisha; tumeondoa TOZO katika huduma ya kutuma pesa chini ya Tshs 200,000 kwenda mitandao yote ya simu kipindi hiki cha maumbukizi ya KORONA,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa benki ya Access katika ukurasa wa Twitter.
Ni dhahiri kuwa wateja wa benki hiyo wanaotumia simu benki wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu benki hiyo imewapatia unafuu.
Soma zaidi:
-
BoT yatoa ufafanuzi noti za Tanzania kusambaza virusi vya Corona
-
Chanjo ya virusi vya Corona yaanza kufanyiwa majaribio
-
Makamba azishauri benki, kampuni za simu kuondoa tozo za simu benki
Machi 19, 2020 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa taarifa kwa umma kuwataka wananchi kutumia mifumo mbadala kufanya malipo ikiwemo kadi, simu na intaneti ili kupunguza matumizi ya noti.
BoT ilieleza kuwa kutokana na noti hizo kupita katika mikono ya watu wengi, zinawaweza kubeba vimelea vya virusi vya Corona na kusambaza ugonjwa huo kwa watu wasiokuwa nao.
Hata hivyo, katika taarifa ya benki hiyo ilieleza kuwa noti zake zimetengenezwa kwa namna ambayo zinaweza kuzuia vimelea vya magonjwa kubaki katika noti hizo.
Katika hatua nyingine, Makamba amesema hatua iliyochukuliwa na benki ya Access ni ya kupongezwa na kuigwa na taasisi nyingine za fedha na kampuni za simu za mkononi ambazo zinafaidika na biashara ya miamala kwa njia ya simu za mkononi.
“Hongereni kwa kuonyesha jinsi sekta binafsi, hasa sekta ndogo ya fedha, inavyoweza kusaidia kwenye jambo hili. Natumaini “wakubwa” kwenye sekta ya benki – @CRDBBankPlc @NMBTanzania @TZ_StanChart @AbsaTanzania na wengine – watafuata njia. @VodacomTanzania @airtel_tanzania @Tigo_TZ,” ameandika Makamba katika ukurasa wake wa Twitter jana.
Makamba ambaye ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga pia ameiomba Wizara ya Afya kuongea na kampuni za bia kuangalia uwezekano wa kuzalisha vitakasa mikono (sanitizers) kwa wingi ili vipatikane kwa urahisi kwa wananchi kujikinga na Corona.
“Ndugu Waziri: kampuni za pombe kali, TBL/TDL (Konyaji), Mega (K-Vant) na nyingine, zinaweza kuambiwa/kuombwa/kusukumwa kuzalisha pia sanitizers na kuzijaza sokoni. Vilevile kwa Mtibwa/Kilombero Sugar na TPC, kunakozalishwa ethanol. Sanitizers zapaswa kuwa rahisi kupata na kununua,” amesema Makamba.
Ndugu Waziri: kampuni za pombe kali, TBL/TDL (Konyaji), Mega (K-Vant) na nyingine, zinaweza kuambiwa/kuombwa/kusukumwa kuzalisha pia sanitizers na kuzijaza sokoni. Vilevile kwa Mtibwa/Kilombero Sugar na TPC, kunakozalishwa ethanol. Sanitizers zapaswa kuwa rahisi kupata na kununua https://t.co/Jm8TWrS4AE
— January Makamba (@JMakamba) March 20, 2020
Makamba alikuwa akimjibu Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile aliyewakaribisha vijana wabunifu wanaoweza kutengeneza sanitizers, ikizingatiwa kuwa mtaani zinauzwa kwa bei ya juu na wananchi wanaweza wasimudu gharama yake.
Kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hadi jana ugonjwa huo umeambukiza watu 234,073 ambapo watu 9,840 wamefariki dunia.