July 8, 2024

Biashara mifugo kwenye minada yapungua Tanzania

Thamani ya mifugo inayouzwa katika minada mbalimbali nchini Tanzania imeshuka kwa Sh240 bilioni katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikichangiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

  • Idadi ya mifugo iliyouzwa mwaka 2019/2020 ilikuwa milioni 3.7 kutoka milioni 3.9 ya mwaka 2018/2019.
  • Thamani ya mifugo iliyouzwa nayo imeshuka hadi Sh1.06 trilioni mwaka 2019/2020 kutoka Sh1.3 trilioni mwaka 2018/2019. 
  • Mvua zachangia kushusha biashara hiyo.  

Dar es Salaam. Thamani ya mifugo inayouzwa katika minada mbalimbali nchini Tanzania imeshuka kwa Sh240 bilioni katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikichangiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mifugo hiyo inajumuisha ng’ombe, kondoo, mbuzi na punda ambao hutumika kama kitoweo na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani. 

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi katia bajeti ya mwaka 2020/2021 zinaeleza kuwa mwaka 2019/2020 mifugo milioni 3.7 yenye thamani ya Sh1.06 trilioni iliuzwa katika minada mbalimbali nchini. 

Idadi na thamani ya mifugo hiyo imepungua kidogo ikilinganishwa na mwaka 2018/2019 ambapo iliuzwa mifugo milioni 3.9 ikiwa na thamani ya Sh1.3 trilioni.

Hiyo ni sawa na kusema thamani ya mauzo ya mifugo hiyo imeshuka kwa asilimia 18.5. 

“Sababu za kushuka kwa biashara hii ni pamoja na mwaka 2019/2020 kuwa na mvua nyingi hivyo kuathiri biashara ya mifugo katika minada,” amesema Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina katika hotuba ya bajeti ya 2020/2021.


Soma zaidi:


Hata hivyo, takwimu za wizara hiyo hazijaeleza mifugo iliyouzwa mwaka 2019/2020 ni hadi mwezi gani, ikizingatiwa kuwa mwaka huu wa fedha unaisha Juni 30. 

Kati ya mifugo iliyouzwa mwaka 2019/2020, mbuzi walikuwa milioni 1.7 ikiwa ndiyo mifugo iliyochangamkiwa zaidi sokoni na wanunuzi na wafugaji.

Ili kuimarisha biashara ya mifugo, Mpina amesema wanaendelea kuhamasisha matumizi ya mizani katika minada na uanzishaji wa ushirika wa wafanyabiashara wa mifugo.

Pia katika mwaka 2020/2021 wizara yake itajenga minada miwili ya upili na mmoja wa mpakani; na kukarabati minada ya upili na mipakani na kuwezesha utekelezaji wa doria sita za mikakati ya kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake.