Biashara yako inayumba? Tumia mbinu hizi kuiimarisha
Biashara ni kazi kama kazi nyingine kwani inahitaji akili, nguvu na maarifa. Kufanikiwa kibiashara yataka utumie akili yako, ujuzi pamoja na nguvu kwa wakati.
- Fanya tathmini soko la bidhaa zako kama linakubalika.
- Punguza utegemezi kwenye biashara yako.
- Hakikisha mtaji wako unakua kila siku.
Dar es Salaam. Dhana ya biashara imejikita katika kubadilishana bidhaa kwa fedha au bidhaa kwa bidhaa. Na ndoto ya watu kufanya biashara ni kutengeneza kipato.
Lakini unawezaje kutengeneza kipato kupitia biashara hiyo?
Biashara ni kazi kama kazi nyingine kwani inahitaji akili, nguvu na maarifa. Kufanikiwa kibiashara yataka utumie akili yako, ujuzi pamoja na nguvu kwa wakati.
Kwa mtu ambaye anataka kuwa mfanyabiashara bora kwa kutengeneza kipato kizuri ni lazima afanye mambo kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na:
Tafuta wazo la biashara
Hapa kama wewe unataka kufanya biashara lazima ujue unataka kufanya biashara ipi?, Je ni biashara ya nguo, kuuza vyakula/nafaka, kuuza matunda, kuuza duka lenye mchanganyiko wa bidhaa?.
Kama ni kimojawapo basi anza kukifanyia uchunguzi hata kwa wale wengine wazoefu ufahamu mahitaji ya biashara hiyo.
Wafanyabiashara wadogo katika Soko la Soni lilipo Wilaya ya Lushoto, mji huo unaokua kwa kasi Tanzania. Lakini soko hilo liko karibu kabisa na stendi ya mabasi ya Wilaya ya Lushoto. picha| K15 Photos.
Jifunze kuhusu soko la biashara yako
Baadhi ya watu hufanya biashara popote bila kujali kama inaweza kumpatia wateja au la. Matokeo yake anashindwa kumudu gharama za kodi za jengo, umeme na hata sehemu anayouzia kwa sababu ya soko la biashara yake kuwa hafifu.
Kwa wale wa biashara za mtandaoni nao pia wanashauriwa kufahamu soko lao lipo mitandao gani zaidi ili kunufaika na wateja.
Linda mtaji wako
Hakikisha unalinda mtaji wako usipotee bali uongezeke ili kuitanua biashara yako. Mfano umeanza na mtaji wa Sh100,000, unachotakiwa kufanya ni kuilinda hiyo hela ili izidsi kujizalisha na kupata faida.
Wakati wa kupanga namna ya kuikuza biashara, usisahau kuimarisha mtaji wako ili hata biashara ikiyumba unaweza kuendelea kuwepo kwenye soko la ushindani.
Tengeneza mipango na jitume
Mfanyabiashara ni lazima ujue faida na hasara zinazoingia kwenye biashara yako ndipo utafute njia mbadala ya kupunguza au hata kuziondoa kabisa hizo changamoto.
Pia jitume, fanya biashara kwa malengo mfano jiwekee kiasi fulani cha faida ambacho lazima ukifikie kila mwezi kwa namna yoyote ile.
Wakazi wa Wilaya ya Mbogwe wakiendelea na shughuli za kuuza bidhaa katika soko la Masumbwe wilayani humo. Picha| Gift Mijoe.
Punguza utegemezi
Kitu kikubwa ambacho huwaangusha wafanyabiashara walio wengi ni kutegemea biashara anayoifanya ili ikidhi mahitaji yake.
Mfano umepanga kwenye nyumba ya kulipia Sh50,000 kila mwezi huku faida ya biashara ndiyo inatumika kulipia kodi na kukidhi mahitaji yote ya nyumbani.
Kama biashara yako haijasimama vizuri, inaweza kuyumba na ukapoteza mtaji wote na kulazimika kukopa fedha ili kuanza upya. Tengeneza vyanzo vingine vya mapato ili kukidhi mahitaji yako.
Tumia vizuri teknolojia
Wakati mwingine biashara zetu hushindwa kuzaa matunda kwasababu ya kutoendana na teknolojia iliyopo, mfano unafanya biashara ya kuuza vyakula au hata nguo, ipeleke mtandaoni ili kufaidika na soko la watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Dondoo hizi zinaweza kukusaidia kupiga hatua katika biashara yako.