November 24, 2024

Bidhaa za mazao zachangia kupaisha mauzo nje ya nchi Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika mwaka ulioishia Machi 2020 imeongezeka kwa asilimia 12.1 yakichagizwa zaidi na bidhaa za mazao ikiwemo korosho na mkonge.

  • Mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi yaliongezeka hadi Sh23.1 trilioni machi 2020 ikilinganishwa na Sh20.3 trilioni Machi 2019.
  • Kuimarika hali ya hewa, bei ya dunia kumesaidia bidhaa za mazao kuuzwa kwa wingi.
  • Corona yashusha mauzo ya jumla ya Machi 2020.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika mwaka ulioishia Machi 2020 imeongezeka kwa asilimia 12.1 yakichagizwa zaidi na bidhaa za mazao ikiwemo korosho na mkonge. 

Mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi hujumuisha bidhaa za mazao na zile zisizo za mazao ikiwemo madini ya dhahabu na almasi. 

Ripoti ya tathmini ya uchumi ya mwezi Machi 2020 iliyotolewa na benki hiyo imesema kwa ujumla mapato yatokanayo na mauzo nje ya nchi yaliongezeka hadi Dola za Marekani 9.95 bilioni (Sh23.1 trilioni) kwa kipindi hicho ikilinganishwa na dola  8.74 bilioni (Sh20.3 trilioni) iliyorekodiwa Machi 2019.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 12.1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja lililochochewa na kupaa kwa thamani ya mauzo ya bidhaa za mazao.

“Thamani ya bidhaa za mazao iliongezeka hadi Dola za Marekani 1.01 bilioni (Sh2.4 trilioni) kwa mwaka ulioishia Machi ikilinganishwa na dola 569.2 milioni (Sh1.3 trilioni) katika kipindi kama hicho mwaka 2019,” imesema BoT.

Mauzo ya bidhaa zote za mazao yaliongezeka katika kipindi hicho isipokuwa kahawa,chai na tumbaku. 

BoT imeeleza kuwa kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za mazao kumechagizwa na hali ya hewa nzuri, ongezeko la uzalishaji na matokeo ya bei nzuri katika soko la dunia. 

Aidha, thamani ya mauzo ya jumla ya bidhaa na huduma nje ya nchi pia yamechangiwa na bidhaa zisizo za mazao ikiwemo dhahabu.

Katika kipindi hicho, mauzo ya dhahabu ambayo yalikuwa zaidi ya nusu au asilimia 55.7 ya bidhaa zisizo za mazao (non-traditional goods) yaliongezeka kwa asilimia 37.9  hadi kufikia dola 2.34 bilioni (Sh5.4 trilioni).

Hata hivyo, mauzo ya bidhaa za viwandani, samaki na bidhaa za samaki yalishuka. 

Corona yavuruga mauzo ya Machi

Wakati mauzo ya bidhaa na huduma katika kipindi cha mwaka mmoja yakiongezeka, mauzo hayo kwa mwezi Machi yamepungua ikilinganishwa na mwezi uliotanguliwa wa Februari 2020.

Mauzo ya jumla yamepungua kutoka dola za Marekani 802.3 milioni (Sh1.8 trilioni) Februari 2020 hadi dola 667.6 milioni (Sh1.5 trilioni) kutokana na kupungua kwa huduma za malipo hasa katika sekta ya utalii. 

Ripoti hiyo imesema ugonjwa wa virusi vya Corona umeathiri biashara ya utalii kwa sababu shughuli za utalii zilisimama kwa muda kutokana na vikwazo vya vya watu kusafiri ili kujikinga na ugonjwa huo.