November 24, 2024

Bilionea wa China ahukumiwa kifungo cha miaka 18 jela

Sun Dawu, bilionea maarufu wa China amehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na kutakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani 480,000 (takriban Sh1.2 bilioni) kwa makosa ya uhalifu unaodaiwa kuchochea vurugu nchini humo.

  • Ni Sun Dawu, anayemiliki biashara ya kilimo na ufugaji.
  • Amehukumiwa kwa makosa ya uhalifu unaodaiwa kuchochea vurugu nchini humo.
  • Pia ametakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani 480,000 (takriban Sh1.2 bilioni).

Sun Dawu, bilionea maarufu wa China amehukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na kutakiwa kulipa faini ya Dola za Marekani 480,000 (takriban Sh1.2 bilioni) kwa makosa ya uhalifu unaodaiwa kuchochea vurugu nchini humo. 

Bilionea huyo ambaye ni Mwenyekiti wa kampuni ya kilimo ya Dawu iliyopo  Kaskazini mwa jimbo la Hebei na muungaji mkono wa harakati za kutetea haki za binadamu alihukumiwa Julai 28, 2021 katika kesi iliyoendeshwa kwa siri.

Kwa mujibu wa mahakama iliyomtia hatiani iliyoko Gaobeidian karibu na jiji la Beijing, Dawu alipatikana na hatia ya makosa ya uhalifu ikiwemo kukusanya watu kushambulia taasisi za kiserikali na kusababisha usumbufu wa shughuli za kijamii na kuchochea matatizo.

Tuhuma hizo zilizompeleka jela bilionea huyo inaelezwa zimekuwa zikutumiwa mara kwa mara dhidi ya wakosoaji wa Serikali ya kikomonisti ya China.

Bilionea huyo alikamatwa na polisi Novemba mwaka jana pamoja na ndugu zake 19 na washirika wake wa kibiashara baada ya kampuni yake kuingia kwenye mvutano wa ardhi na kampuni inayomilikiwa na serikali ambayo ni mshindani wake kibiashara. 

Kampuni hiyo ya Serikali ilijaribu kuvunja majengo ya kampuni ya Dawu lakini wafanyakazi wake waliingilia kati na kuzuia shughuli hiyo, jambo lililozua vurugu.

Kampuni anayomiliki Dawu ni miongoni mwa kampuni kubwa nchini China ambazo zinahusika na uchakataji wa nyama na vyakula vya wanyama shuleni na hospitalini.

Hii siyo mara ya kwanza kwa bilionea huyo kufungwa jela. Mwaka 2003 alifungwa kwa makosa ya kuchangisha fedha kinyume na sheria lakini baadaye alishinda kesi hiyo.