Bima ya afya iliyoboreshwa kupunguza ramli chonganishi Shinyanga
Wananchi wa mkoa huo wamehimizwa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) ili kupata uhakika wa matibabu katika vituo vya afya na kuachana na tiba zisizothibitishwa.
- Wananchi wa mkoa huo wamehimizwa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) ili kupata uhakika wa matibabu katika vituo vya afya.
- Mfuko utawasaidia kuepuka kwenda kupiga ramli.
Dar es Salaam. Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) ili kupata uhakika wa matibabu katika vituo vya afya na kuachana na fikra za kwenda kupiga ramli chonganishi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizindua kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo katika kijiji cha Ilobashi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, amesema bima ya afya inawasaidia wananchi kuwa na uhakika wa matibabu kwa bei nafuu kwa mwaka mzima.
Amesema wananchi wakiwa na uhakika wa matibabu hata wakipatwa na maradhi hawatakuwa na mawazo ya kwenda kupiga ramli chonganishi kwa sababu tayari wana vitambulisho,.Tusirudi huko ndugu zangu, kwenye kupiga ramli,” amesisitiza Telack.
Amewaasa pia wananchi ambao vitambulisho vyao vimekwisha muda wake walipie tena kwa mwaka huu ili waendelee kupata matibabu huku akiwakumbusha Waganga Wafawidhi wa vituo vyote vya afya mkoani humo kuhakikisha dawa na vifaa vinakuwepo.
“Serikali inataka Watanzania wote wanakuwa na bima za afya ili kuweza kutibiwa kwa wakati, ubora na kwa bei nafuu, hakikisheni madirisha ya wagonjwa wa CHF yanakuwepo na yanafanya kazi kama ilivyo kwa madirisha ya wazee,” amesema Telack.
Soma zaidi: Moto, afya, vyombo vya moto vinavyotawala soko la bima Tanzania
Mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa mitatu nchini ambayo mradi wa CHF umetekelezwa ambapo wananchi 25,513 kati ya 261,608 wameshajiunga na mfuko huu tangu ulipozinduliwa rasmi mkoani humo Oktoba 4, 2018. Mikoa mingine ni Dodoma na Morogoro.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliyembatana na Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi huo, amewasisitiza wakulima wote kujiunga na mfuko huo mara tu watakapouza pamba ili wawe na uhakika wa matibabu.
“Kazi ya kilimo ina mchango mkubwa kwa pato la Taifa, asilimia 28.7 inatokana na kilimo, hivyo siku hii ni muhimu sana kwa wakulima na mimi nasema, huwezi kulima kama huna afya nzuri” amesema Hasunga.