October 6, 2024

Biogesi inavyosaidia kudumisha ndoa Tanzania

Ni Christina Mwanga mkazi wa kijiji cha Olevolos kilichopo kata ya Kimnyaki nje kidogo ya jiji la Arusha, Tanzania ambaye anatumia nishati ya biogesi (Biogas) kwa ajili ya kupikia.

  • Ni nishati ya kupikia inayompunguzia muda na gharama za kuandaa chakula cha familia.
  • Sasa amepunguza gharama za kununua kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
  • Anatumia kinyesi cha nguruwe anaowafuga nyumbani kwake kama malighafi ya kuzalisha biogesi. 

Dar es Salaam. Ukimtazama usoni ni mwenye tabasamu na bashasha. Tabasamu hilo, kwa mujibu wa mama huyu mwenye miaka 39, linatokana na utulivu wa kiakili alionao unaomuwezesha kutimiza majukumu ya nyumbani bila wasiwasi.

Hana mawazo tena ni wapi atapata nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia chakula cha familia. Mume na watoto wake hawasubiri muda mrefu tena kupata chakula na maji ya moto ya kuoga.

Huyo ni Christina Mwanga mkazi wa kijiji cha Olevolos kilichopo kata ya Kimnyaki nje kidogo ya jiji la Arusha, Tanzania ambaye anatumia nishati ya biogesi (Biogas) kwa ajili ya kupikia.

“Biogesi imenipa utulivu. Nina utulivu wa kisaikolojia siwazi tena nikiwa kwenye shughuli zangu hata kama nimechelewa kurudi nyumbani usiku…siwazi kwamba itakuaje sina kuni, mpaka nikawashe moto wa mkaa, hapana,” anasema Christina.

Christina ameiambia nukta (www.nukta.co.tz) hivi karibuni katika makazi yake Arusha yaliyozungukwa na mazingira tulivu ya miti ya migomba aina tofauti ya ndizi iliyonawiri kutokana na kukuzwa kwa samadi itokanayo na mabaki ya taka. 

Christina, ambaye ni mfugaji wa nguruwe, ni miongoni mwa Watanzania wachache wanaotumia biogesi kama nishati mbadala na safi ya kupikia nchini Tanzania. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2016 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) matumizi ya biogesi katika kaya za Tanzania yapo chini ya asilimia moja huku wengi wakitumia zaidi kuni na mkaa katika shughuli za nyumbani. 

Biogesi ni nishati ya kupikia, kutoa mwanga na uzalishaji viwandani inayotokana na mabaki ya mimea na vinyesi vya wanyama. Mabaki hayo hukusanywa na kuwekwa katika eneo maalum kabla ya kuchakatwa na kutumika kuzalisha nishati hiyo katika mtambo maalum wa biogesi kwa ajili ya matumizi mbalimbali. 

Kinyesi maarufu kwa kuzalisha biogesi, kwa mujibu wa watalaamu wa kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (Camartec), ni pamoja na cha ng’ombe, nguruwe, kuku, binadamu na mbuzi lakini kinachotumika zaidi ni cha nguruwe na ng’ombe kwa sababu kina virutubisho vingi kuzalisha nishati hiyo. 

Baadhi ya nguruwe anaofuga Christina ambao awatumia kama biashara na kinyesi chao hutumika kuzalisha nishati ya biogesi kwa ajili ya kupikia chakula nyumbani. Picha|Daniel Samson.

Tulizo kwa wanawake

Jamii nyingi za wanawake waishio vijijini, hutumia muda mwingi kutafuta maji, kuni na mkaa kwa ajili ya shughuli za nyumbani, jambo linalopunguzia kasi yao ya kujiletea maendeleo ikilinganishwa na wanaume na pia wenzao wa mijini.

Lakini Christina ambaye ni mama wa nyumbani mwenye mume na watoto watatu kwake nishati ya uhakika ya kupikia siyo changamoto tena kwa sababu tayari ana mtambo wa kuzalisha biogesi nyumbani kwake. 

Mama huyo, ambaye anatumia biogesi kwa miaka minne sasa ameiambia Nukta kuwa nishati hiyo siyo tu inamuwezesha kupika chakula kwa haraka bali imemsaidia kuokoa muda aliokuwa anatumia kutafuta kuni na mkaa. 

“Kwanza inaniokolea muda, mimi kama mwanamke nina shughuli nyingi za kufanya kwa hiyo nikataka kupika situmii muda mrefu kwa ajili ya kupika kwa sababu biyogesi inaniokolea muda,” anasema Christina huku akiendelea na shughuli za kukusanya kinyesi katika mabanda yake ya nguruwe. 

Christina, ambaye pia kitaaluma ni mwalimu wa waalimu, sasa ana ujasiri wa kukiri kuwa mahusiano na familia yake yameimarika zaidi tangu aanze kutumia nishati hiyo. 

Anasema mume na watoto wake wakiamka asubuhi wanapata maji ya kuoga na kifungua kinywa ndani ya muda na kuwahi katika shughuli zao, kwa sababu hawasubiri tena mpaka moto wa mkaa uwashwe kwa dakika 30.

“Biogesi imenisaidia kwenye mahusiano yangu na familia. Kwa mfano mume wangu akitaka maji ya kuoga anayapata kwa muda anaoutaka, akitaka chakula anapata kwa muda anaoutaka,” anasema mama huyo.

Gharama za kununua na kusafirisha gesi ya majumbani na kuni sasa hazimuumizi tena kichwa Christina na fedha anazozipata anazitumia katika shughuli nyingine za maendeleo.

Anasema hapo awali alikuwa anatumia zaidi ya Sh70,000 kwa mwezi kununua gesi ya kawaida na mkaa kwa ajili ya kupikia. 

“Halafu zile kuni nikutumia mara nyingi unapata moshi, vurugu za kila namna uchafu kwa wingi lakini tangu nimeanza kutumia biogesi mazingira yangu ni masafi, sufuria zangu ni safi,” amesema. 

Hata hivyo, Christina hakupata ujanja huo hewani. Baada ya kuelimishwa faida za biogesi, hana gharama zozote zaidi ya kukusanya kinyesi cha nguruwe na kukiweka kwenye mtambo ambao unampatia nishati moja kwa moja katika jiko lake lililo pembeni ya nyumba yake. 

 

Kwanini kinyesi cha nguruwe?

Christina ambaye anamiliki nguruwe saba mpaka sasa kwa ajili ya shughuli za kibiashara anasema amebaini kuwa moto wa kinyesi cha mnyama huyo una nguvu kubwa ukilinganisha na wanyama wengine. 

Anasema kwa sababu alianza kufuga nguruwe kabla ya kufungiwa mtambo wa biogesi, ilimrahisishia kutumia rasilimali alizonazo kujifaidisha na siyo kutafuta kinyesi cha ng’ombe. 

Ukiachana na Christina aliyekuwa akifuga nguruwe tangu awali, Mhandisi wa nishati ya biogesi kutoka Camartec jijini Arusha, Nicholaus Mwakisambwe amesema kinyesi hicho kina nguvu zaidi kuzalisha gesi nyingi kuliko cha ng’ombe licha ya kuwa upatikanaji wake siyo mkubwa kuliko cha ng’ombe. 

“Kilo moja ya kinyesi cha ng’ombe inatoa lita za ujazo 45 za gesi, kilo moja ya kinyesi cha nguruwe inatoa lita 60 ya gesi. Kwa binadamu na kuku kilo moja inaweza kuzalisha hadi lita 70. 

“Ng’ombe mmoja kwa siku anaweza kuzalisha kilo 12 (za kinyesi) lakini ukija kwenye nguruwe anazalisha kilo nne lakini kina nguvu zaidi,” amesema Mwakisambwe. 


Soma zaidi: Maoni: 


Camartec ambayo imekuwa ikichagiza matumizi ya biogesi nchini Tanzania imefanikiwa kufunga mitambo zaidi ya 12,000 kwenye kaya, shule na taasisi mbalimbali na kutoa mafunzo kwa mafundi 500 wanaotoa huduma kwa wananchi nchi nzima. 

Mtaalam huyo wa biogesi amesema ufungaji wa mitambo ya biogesi hutegemea zaidi ukubwa wa kaya, taasisi, upatikanaji wa vifaa na malighafi na eneo alipo mtu au taasisi.

Mathalani, mtambo mdogo wa lita za ujazo sita ambao unafaa familia yenye watu wanne, amesema unafungiwa kwa gharama ya Sh1.8 milioni hadi Sh2 milioni. 

Mtambo wa lita za ujazo tisa ambao ni mahususi kwa familia ya watu watano hadi nane gharama yake ni Sh2.2 milioni hadi milioni 2.7 na mtambo wa lita za ujazo 13 kwa kaya yenye watu tisa hadi 15 ni Sh2.8 milioni hadi Sh3 milioni. 

Mwakisambwe amesema gharama hizo hujumuisha malighafi na vifaa vyote vinavyohitajika pamoja na elimu ya jinsi ya kutumia kwa usahihi mtambo wa biogesi. 

Christina akiwasha jiko la biogesi tayari kwa kuanza maandalizi ya chakula cha mchana, jiko ambalo anatumia kupika vyakula vyote na hana mpango tena wa kutumia kuni na mkaa. Picha|Daniel Samson.

Changamoto za matumizi biogesi

Christina amesema baada ya kufungiwa mtambo huo, hakuna gharama yoyote ya matengenezo aliyoipata lakini changamoto kubwa ni kuwa majiko ya gesi hiyo anayotumia hayadumu muda mrefu.

Amesema kila mwaka analazimika kununua jiko lingine ili aendelee kufaidika na biogesi ambalo bei yake ni kati ya Sh80,000 na Sh150,000 inategemea na ama yametoka ndani au nje ya nchi. 

Hata hivyo, Mhandisi Mwakisambwe amesema wameanza kutengeneza majiko imara hapa Tanzania ambayo bei yake iko juu kidogo kuliko yanayotumika sasa ambayo mengi yanaagizwa kutoka nje ya nchi. 

Matarajio aliyonayo kwa wanawake wenzake

Christina anasema anapenda kuona teknolojia hiyo inawanufaisha wanawake wengi hasa wa vijijini ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa. 

Anakusudia kuboresha mtambo wake ili aanze kuwasambazia nishati hiyo majirani zake na wao wawe sehemu ya kutunza mazingira ya kijiji chake na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa. 

Hata hivyo, ameiomba Serikali kuliangalia suala hilo na kufadhili miradi ya biogesi ili kuwaletea wananchi hasa wanawake ahueni ya maisha kwa sababu bei za kufunga mitambo ziko juu na watu wengi hasa maskini hawawezi kumudu gharama zake kwa wakati mmoja.