November 24, 2024

Bodi mpya ya korosho mbioni kutangazwa

Serikali imesema inakamilisha muundo mpya wa bodi hiyo ikiwemo uteuzi wa mwenyekiti wake.

Korosho ina upekee wake katika maisha ya watanzania hasa wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kwa kuwa hutegemea zao hilo kujiingizia kipato ambacho hutumika kutunza familia na kusomesha watoto ili kuondokana na umaskini katika jamii. Picha| Mtandao.


  • Serikali imesema inakamilisha muundo mpya wa bodi hiyo ikiwemo uteuzi wa mwenyekiti wake. 
  • Tayari wajumbe nane wa bodi hiyo wameteuliwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu. 
  • Bodi ya zamani ilivunjwa kwa kushindwa kusimamia maendeleo ya zao la korosho.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema Serikali inakamilisha uundaji wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (TCB) ikiwemo uteuzi wa mwenyekiti wake na itatangazwa muda mfupi ujao. 

Hatua hiyo inakuja baada ya miezi saba tangu, Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mama Anna Abdallah na kuivunja bodi hiyo Novemba 10, 2018.

Mgumba ametoa kauli hiyo bungeni leo (Mei 24, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Sikuzani Chikambo ni lini Serikali itachukua hatua tena ya kuunda Bodi ya Korosho na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kwa mazao mengine.

“Serikali inakamilisha uundaji upya Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, kuteua wajumbe kutatangazwa na mamlaka za uteuzi muda mfupi ujao kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni zilizopo,” amesema Mgumba.  


Zinazohusiana:   


Naibu Waziri huyo, amesema taratibu za kukamilisha muundo mpya wa bodi hiyo unaendelea na itatangazwa baada ya Mwenyekiti wake kuteuliwa ambapo wajumbe wake wamepatikana tayari.  

“Mnamo Aprili 15, 2019, Waziri wa Kilimo alimteua Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho na wajumbe nane wameshateuliwa kwa kipindi cha miaka mitatu,”. 

Wakati wa kuivunja bodi ya zamani, Rais Magufuli alisema bodi hiyo ilishindwa kusimamia kikamilifu majukumu yake ikiwemo bei ya korosho katika msimu wa 2017/2018 na kuendeleza zao hilo la biashara linaloongoza kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.