November 24, 2024

Bodi ya mazao mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima

Mpaka sasa Serikali imefanikiwa kukusanya tani 181,000 za korosho ikiwa zimepita zaidi ya wiki tatu tangu ilipositisha ushiriki wa wanunuzi binafsi kuchukua korosho kutoka kwa wakulima.

Baada ya kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora na mkulima aliyepeleka ndiye mwenyewe. Majaliwa amesema ndipo taratibu za malipo hufanyika. Picha| Royal Nuts Kenya.


  • Serikali kupitia Bodi ya nafaka na  mazao mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima nchini ambazo zitabaki bila ya kununuliwa.
  • Mpaka sasa imefanikiwa kukusanya tani 181,000 za korosho ikiwa zimepita zaidi ya wiki tatu tangu ilipositisha ushiriki wa wanunuzi binafsi kuchukua korosho kutoka kwa wakulima.

Dar es Salaam. Serikali imesema mpaka sasa imefanikiwa kukusanya tani 181,000 za korosho ikiwa zimepita zaidi ya wiki tatu tangu ilipositisha ushiriki wa wanunuzi binafsi kuchukua korosho kutoka kwa wakulima na kuwahakikishia kuwa korosho zao zote zitanunuliwa baada ya kujiridhisha kama kweli zimezalishwa nchini na zina ubora unaokubalika. 

Novemba 12 mwaka huu, Rais John Magufuli  alisema Serikali itanunua shehena yote ya korosho inayokadiriwa kufikia tani 220,000 na kuzitafutia soko nje ya nchi baada ya wanunuzi binafsi kuainisha bei ndogo ya kununua zao hilo linalotegemewa zaidi na wakulima wa mikoa ya Kanda ya Kusini.

“Nimeamua kusitisha mnada na sasa Serikali itanunua yenyewe kwa gharama ya Sh3,300 kwa kilo,” alisema Rais Magufuli  aliyekuwa akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri wapya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mapema leo (Desemba 7, 2018), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra akiwa njiani kwenda Dodoma amewatoa hofu wakulima na kuwahakikishia kuwa korosho zao zote zitanunuliwa.

Amesema Serikali kupitia Bodi ya nafaka na  mazao mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho za wakulima nchini ambazo zitabaki bila ya kununuliwa na bodi hiyo inaendelea kufanya tathmini na kujiridhisha kama kweli korosho hizo zimezalishwa nchini na kuangalia viwango vya ubora.

Baada ya kujiridhisha kuhusu viwango vya ubora na mkulima aliyepeleka ndiye mwenyewe. Majaliwa amesema ndipo taratibu za malipo hufanyika.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha mkulima ananufaika na ndipo Rais Dkt. John Magufuli alisitisha ununuzi baada ya kuona wakulima wanataka kudhulumiwa,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, hadi sasa tayari tani 181,000 zimeshakusanywa ambapo wakulima wanaolima zao hilo nchini wametakiwa waendelee kuiamini Serikali yao.

Meneja Utawala wa kiwanda cha Terra, Peter Ngwale alisema uwezo wao ni kubangua tani 6,000 kwa mwaka, ambapo tayari wamebangua tano 3,000.

Pia aliiomba Serikali iwasaidie katika suala la ubora wa korosho kwa kuwa kiwango cha ubora kinachoandikwa kinakuwa tofauti na uhalisia wa korosho  yenyewe.

Licha ya kuwepo viwanda vichache vya kubangua korosho, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof Joseph Buchweishaija wakati akihojiwa na gazeti la Mwananchi alisema mpango wa Serikali ni kuhakikisha korosho iliyokusanywa inabanguliwa hapa nchini.

Alisema tayari wameliagiza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (Tirdo) kufanya tathmini na kubainisha mahitaji yatakayofanikisha ubanguaji wa korosho hapa nchini.