October 8, 2024

Bodi ya mikopo yaanza kutekeleza madai ya wanafunzi UDSM

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) imeanza kuyafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) likiwemo la kuwapatia mikopo wanafunzi waliobadilisha kozi ambapo wataingiziwa fedha zao D

  • Imesema wanufaika waliopata changamoto, wataanza kuingiziwa fedha zao wiki hii.
  • Wanafunzi watakiwa kuwasilisha changamoto zao katika menejimenti za vyuo vyao kabla ya kwenda Heslb.
  • Daruso yasisitiza kufika katika ofisi za Heslb kudai haki za wanafunzi.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) imeanza kuyafanyia kazi madai yaliyotolewa na Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) likiwemo la kuwapatia mikopo wanafunzi waliobadilisha kozi ambapo wataingiziwa fedha zao Desemba 18, 2019 baada ya kukamilisha uchambuzi wa taarifa zao. 

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kutoa saa 72 kwa bodi hiyo kutekeleza maagizo manne likiwamo kuwaingizia fedha wanafunzi ambao hawajapewa tangu chuo hicho kifunguliwe.

Taarifa ya Daruso iliyotolewa Desemba 15, 2019 ilieleza kuwa endapo maagizo hayo hayatatekelezwa katika muda uliotolewa wanafunzi watakusanyika nje za ofisi za Heslb, zilizopo Mwenge jijini Dar es Salaam kupigania hatma yao. 

Daruso imedai kuwa walifikia uamuzi huo baada ya wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza kukosa mikopo tangu chuo kifunguliwe huku baadhi ya wanafunzi wanaoendelea wakikatwa fedha zao. 

Daruso pia imeitaka Heslb kurejesha makato ya fedha za vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Heslb, Abdul-Razaq Badru aliyekuwa akizungumza jana (Desemba 16, 2019) jijini Dar es Salaam katika kikao kati yake menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wawakilishi wa viongozi wa Daruso, amesema wanafunzi waliobadilisha kozi wataingiziwa fedha zao baada ya mchakato wa malipo kukamilika. 

“Kuna kundi la wanafunzi waliobadilisha kozi wakiwa vyuoni na taarifa zilikuwa bado hazijatufikia, tumezipokea mwishoni mwa wiki na tunakamilisha malipo ambayo yatawafakia siku mbili zijazo,” amesema Badru katika taarifa ya Heslb.

#Ufafanuzi
pic.twitter.com/idlpfszpVs

Akizungumzia malipo ya vitabu, mafunzo kwa vitendo na utafiti, Badru amesema tayari awamu ya kwanza malipo imefanyika na awamu ya pili itafanyika Desemba 21 kwa wanafunzi ambao bado hawajapata baada ya wataalam wa Heslb kukamilisha uchambuzi.

“Kundi jingine linahusu malipo ya vitabu na viandikwa ambapo awamu ya kwanza ya malipo ya jumla ya Sh13.3 bilioni yameshafanyika na awamu ya pili ya Sh1.1 bilioni itawafikia wanafunzi ifikapo jumamosi ijayo Desemba 21 mwaka huu kwa kuwa wataalam wetu wanakamilisha uchambuzi,” amesema Badru katika kikao hicho.

Bodi hiyo imevitaka vyuo vikuu nchini kuimarisha mifumo ya mawasiliano na serikali za wanafunzi ili kurahisisha upokeaji na utatuzi wa changamoto wanazozipata wakati wa kupata mikopo ya kujikimu wakiwa vyuoni.  

Kwa mujibu wa Heslb, hadi sasa wanafunzi 49,485 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo yenye thamani ya Sh169.4 bilioni na kuvuka lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka kwanza wapatao 45,000.

Hata hivyo, Daruso kupitia akaunti yake ya Twitter imeeleza kuwa ni kweli viongozi wake akiwemo Rais wake, Hamis Musa walihudhuria kikao hicho lakini siyo hoja zao zote zilipatiwa ufumbuzi na msimamo wao kwenda katika ofisi za Heslb keshokutwa Desemba 19, 2019 uko pale pale. 


Zinazohusiana


Wanufaika wa mikopo watahadharishwa

Katika hatua nyingine, Heslb imewataka wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wanaokumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupata mikopo yao kuwasiliana na menejimenti za vyuo vyao kwanza ili zipatiwe ufumbuzi haraka. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Heslb, Profesa William Anangisye akizungumza katika kikao hicho amesema ni vema wanufaika wa mikopo kufuata njia sahihi wakati wakidai haki zao.

“Wanafunzi wote wa taasisi za elimu ya juu wanapokutana na changamoto wasisite kuziwasilisha kwa menejimenti za vyuo ambazo zitawasilishwa Heslb au kwa taasisi sahihi, hata nyie (Daruso) mlipaswa kuanzia kwetu tungeyafanyia kazi yote badala ya kutoa maelekezo ya masaa 72,” amesema Prof. Anangisye katika taarifa hiyo ya Heslb.