July 3, 2024

Bosi mpya wa Tanroads huyu hapa

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Rogatus Mativila kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) akichukua nafasi ya marehemu Mhandisi Patrick Mfugale.

  • Ni Rogatus Mativila.
  • Mativila alikuwa Mkurugenzi wa Barabara Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
  • Anachukua nafasi iliyoachwa na  marehemu Mhandisi Patrick Mfugale.

Mwanza. Hatimaye kitendawili cha mrithi wa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) iliyokuwa inashikiliwa na marehemu Mhandisi Patrick Mfugale kimeteguliwa leo baada ya uteuzi kufanyika.

Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amemteua Rogatus Mativila kushika nafasi hiyo, uteuzi ambao umeanza jana 28, 2021.

Mativila amechukua nafasi ya marehemu Mhandisi Mfugale aliyefariki dunia Juni 29 mwaka huu. 

Kabla ya uteuzi huo,  Mativila alikuwa Mkurugenzi wa Barabara Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya ujenzi) na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanroads. 

Bosi huyo mpya wa Tanroads atakuwa na kibarua kigumu cha kuendeleza kazi kubwa  iliyofanywa na mtangulizi wake ambaye alikuwa nguzo muhimu katika sekta ya ujenzi nchini.

Mfugale atakakumbukwa  kwa kusimamia usanifu na ujenzi wa barabara na madaraja zaidi ya 1,000 nchini. 

Kuenzi mchango wake katika ujenzi wa miundombinu, mwaka 2018 Hayati Rais John Magufuli aliagiza daraja la juu la Ubungo la jijini Dar es Salaam. lipewe jina la Mhandisi Mfugale (Mfugale Flyover) 

Katika hatua nyingine  Rais Samia amemteua Profesa Yunus Mgaya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ya Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico). 

Kabla ya uteuzi huo,  Prof Mgaya alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr).