BoT yaeleza sababu za kuchelewa kununua dhahabu Tanzania
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga ameeleza sababu mbalimbali za benki hiyo kuchelewa kuanza kununua dhahabu kama sehemu ya hifadhi zake (gold reserve) ikiwemo kutokuwepo kwa viwanda vya kuongeza thamani madini hayo nchini.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof Florens Luoga akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa BoT leo jijini Dar es salaam kuhusu umuhimu wa kutumia Noti safi kushoto ni Julian Banzi Raphael Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani. Picha|Daniel Samson.
Yasema kutokuwepo kwa viwanda vya kuongeza thamani madini hayo kumechangia zoezi hilo kuahirishwa.
- Yasema haitanunua dhahabu kwenye minada ili kuhakikisha ubora wa madini hayo.
- Yasema inaweka utaratibu mzuri na ndani ya miaka mitano itakuwa na hifadhi ya kutosha ya dhahabu.
Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga ameeleza sababu mbalimbali za benki hiyo kuchelewa kuanza kununua dhahabu kama sehemu ya hifadhi zake (gold reserve) ikiwemo kutokuwepo kwa viwanda vya kuongeza thamani madini hayo nchini.
Januari 10, 2019, Rais wa Tanzania John Magufuli aliitaka BoT kuanza mchakato wa kuanzisha hifadhi ya dhahabu, jambo litakalosaidia Serikali kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa madini nje ya nchi na kusaidia kuimarisha Shilingi pale itapopata mtikisiko.
Hata hivyo, Prof. Luoga amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo kuwa ununuzi wa dhahabu kwa ajili ya akiba ni suala linalohitaji utaratibu mzuri ili likifanyika lifanikiwe na kuhakikisha dhahabu itakayonunuliwa ina ubora wa hali ya juu.
“Tumechelewa kununua dhahabu kwa sababu hakuna refinery machines (viwanda vya kuongeza thamani ya dhahabu). Hatuwezi kununua kwenye minada kwa sababu unatakiwa uzingatie ubora ili kuepuka hasara,” amesema gavana huyo.
Kukosekana kwa viwanda hivyo, kumesababisha dhahabu kusafirishwa nje ya nchi na kisha kurudishwa tena katika masoko ya ndani, jambo ambalo limekuwa likiikosesha Serikali ya Tanzania mapato.
Amesema ikiwa wawekezaji watachangamkia fursa ya kujenga viwanda vya kuchenjua dhahabu nchini, itasaidia upatikanaji wa dhahabu yenye ubora na kuwarahisishia kununua kwa wingi.
“Tunataka tuinue soko la ndani la dhahabu,” amesema Prof. Luoga akibainisha kuwa BoT inataka kuwa sehemu ya kuinua uchumi wa nchi hivyo haiwezi kununua dhahabu ya nje wakati ndani iko kwa wingi lakini kinachohitajika ni kuzingatiwa kwa viwango vya ubora.
Zinazohusiana:
- Maadhimisho ya Tanzanite yaahirishwa kupisha maombelezo ajali ya Mv Nyerere.
- Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
- Uzalishaji wa dhahabu Acacia washuka
Aidha, amesema mchakato wa kuandaa utaratibu mzuri wa ununuzi wa dhahabu unaendelea na katika kipindi cha miaka minne hadi mitano BoT itakuwa na hifadhi ya dhahabu ya kutosha.
“Miaka minne, mitano ijayo tutakuwa na gold reserve (hifadhi ya dhahabu), Itakuwa ya kitaalamu zaidi kwa sababu hatutaki kufanya hicho kitu bila malengo lakini tunataka kugusa soko la ndani na kuongeza mapato serikalini,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Prof Luoga walikubaliana na nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa kiasi cha dhahabu kinachotakiwa kuhifadhiwa kinatakiwa kiwe na uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa miezi minne na nusu.
Kwa upande wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), hifadhi hiyo inatakiwa iwe na uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa miezi sita.
Prof Luoga amesema hifadhi ya dhahabu inaweza kuisaidia nchi wakati wa dharura kama uwepo wa janga kubwa la kiuchumi ambalo linahitaji hatua za haraka kunusuru hali za wananchi.
Madini yamekuwa na mchango muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambapo sekta hiyo inachangia karibu asilimia 4.8 ya Pato la Taifa kutokana na mauzo yanayouzwa nje ya nchi.
Ripoti mpya ya mapitio ya uchumi ya Januari 2020 (Monthly Economic Review) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inabainisha kuwa mapato ya dhahabu iliyouzwa nje ya nchi yaliongezeka hadi Dola za Marekani 2.22 bilioni (Sh5.08 trilioni) mwaka 2019 kutoka Dola za Marekani 1.52 bilioni (Sh3.5 trilioni) mwaka 2018.