July 5, 2024

BoT yaiweka China Commercial Bank chini ya uangalizi

Katika kipindi hicho cha usimamizi kilichoanzia leo (Novemba 19, 2020), amesema benki hiyo itafungwa na haitatoa huduma yeyote kwa wateja mpaka pale BoT itakapotoa maelekezo.

  • Yamteua msimamizi atakayeisimamia benki hiyo kwa siku 90.
  •  Benki hiyo inaingia kwenye orodha ya benki zilizopata misukosuko ya kifedha miaka ya hivi karibuni.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeiweka Benki ya China Commercial Bank chini ya usimamizi wake kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya ukwasi.   

Gavana wa BoT, Florens Luoga amewaambia wanahabari jijini Dodoma kuwa uamuzi huo ni moja ya hatua za kisheria zitakazosaidia kulinda maslahi ya wateja wakati ikitafutwa njia itakayoisaidia benki hiyo kurejesha uwezo wa kuendesha shughuli za kibenki ama kwa kujiendesha yenyewe au chini ya usimamizi wa benki nyingine ya biashara.  

Kwa mujibu wa kanuni za mabenki na taasisi za fedha zinazosimamia masuala ya mitaji za mwaka 2015 (The Banking and Financial Institutions Capital Adequacy (Amendment) Regulations, 2015) benki inatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Sh15 bilioni.


Zinazohusiana:


Kutokana na uamuzi huo wa kiudhibiti, Prof Luoga amesema BoT imeisimamisha bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya benki hiyo na kuteua msimamizi atakayeisimamia kwa siku zisizozidi 90.

Msimamizi huyo katika siku hizo zisizozidi 90 ataingalia namna bora ya kuibadilisha na kuiendesha benki hiyo na baadaye BoT itaamua kitakachofuata.

Katika kipindi hicho cha usimamizi kilichoanzia leo (Novemba 19, 2020), amesema benki hiyo itafungwa na haitatoa huduma yeyote kwa wateja mpaka pale BoT itakapotoa maelekezo.

“Tunatoa taarifa hii ili kusije kuwa na taharuki. Hizi ni taratibu za kawaida ili kuhakikisha tunalinda maslahi ya wateja wa benki hii,” ameeleza Prof Luoga akiongeza kuwa lengo la uamuzi huo siyo kuifilisi benki hiyo yenye makazi yake makuu makutano ya Mtaa wa Ohio na Garden jijini Dar es Salaam.

China Commercial Bank inaingia katika orodha ya benki ambazo zilishawahi kuwekwa chini ya uangalizi wa BoT baada ya kushindwa matakwa ya kimtaji.

Katikati mwa mwaka 2018 BoT iliiweka Bank M katika usimamizi wake baada ya kubaini kuwa taasisi hiyo ya kifedha ilikuwa na mapungufu makubwa ya kimtaji.