October 6, 2024

BoT yatahadharisha huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni

Imesema utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma hizo.

  • Imesema utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali za za fedha (black-market). 
  • Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya BoT kufanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam na kubaini mengi yanajiendesha pasipo kuwa na leseni.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali ikiwemo kuibiwa au kupewa fedha bandia. 

Imesema utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali za za fedha (black-market). 

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya BoT kufanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa maduka mengi yanaendesha biashara hiyo pasipo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BoT leo (Februari 28, 2019), kufuatia ukaguzi huo, Benki Kuu ya Tanzania imeanza utaratibu wa kufuta leseni za maduka yote yaliyokutwa yanaendesha biashara hiyo bila kuzingatia masharti ya leseni.  

“Mnamo mwezi Desemba mwaka 2018, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini kote na kubaini kuwa mengi hayakidhi matakwa ya kisheria ya biashara hiyo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 


Zinazohusiana:


Taarifa hiyo inaeleza kuwa BoT iliyaandikia maduka hayo kuyataka kutoa maelezo kwa nini yasifutiwe leseni kutokana na ukiukaji huo ambapo hatua zilizochukuliwa jana za kukagua zinatokana na tathmini ya taarifa ambazo Benki Kuu ya Tanzania ilizipokea kutoka kwa waendeshaji wa maduka hayo. 

Aidha, huduma za kubadilisha fedha za kigeni zinaendelea kupatikana katika mabenki na taasisi za fedha nchini kote pamoja na maduka ya fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).