Bunge lahoji Serikali kutojenga bandari ya Bagamoyo
Spika Job Ndugai ameitaka itoe ufanunuzi wa kina kwa nini imesitisha ujenzi wa bandari hiyo muhimu Afrika Mashariki.
Muonekano wa mchoro wa bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ambayo inatajwa kuwa itafungua fursa mbalimbali za kiuchumi Afrika Mashariki. Picha|Mtandao.
- Wamehoji leo bungeni wakati wa uchangiaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2019/2020.
- Spika Job Ndugai ameitaka itoe ufanunuzi wa kina kwa nini imesitisha ujenzi wa bandari hiyo muhimu Afrika Mashariki.
Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isach Kamwelwe kutoa ufanunuzi wa sababu za Serikali kusitisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ikizingatiwa kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Taifa.
Akizungumza bungeni leo (Mei 13, 2019) wakati wa uchangiaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2019/2020 amesema haelewi sababu za mradi wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kukwama na amemtaka Mhandisi Kamwelwe kutoa ufafanuzi wa kina wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake leo jioni.
“Sielewi nini kimekwamisha mradi huu wa Bagamoyo labda kama Waziri atapata muda anaweza akatufafanulia vizuri yeye yuko katika nafasi nzuri ya kuelezea jambo hili,” amesema Ndugai.
Amesema huenda kuna sababu za msingi zinazokwamisha mradi huo lakini ni vema Serikali ikaupa kipaumbele mradi huo ambao utafungua fursa nyingi za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo ujenzi wa viwanda na ukuaji wa biashara.
“Narudia tena sijui kilichoko serikalini inawezekana kuna mambo ya msingi sana ya kutazamwa lakini ni kitu ambacho ni vizuri tukakipa macho mawili tukaacha mambo mengine yote, mradi kama huu ni uchumi mkubwa, tukafungua uchumi tukambana jirani yetu (bandari ya Mombasa) anayetukaba kaba kila wakati,” amesisitiza Ndugai.
Zinazohusiana:
- Zanzibar, kitovu utengenezaji wa meli Afrika Mashariki
- Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai
- Meli mpya Ziwa Victoria kuchochea biashara Afrika Mashariki
Amewataka wafanya maamuzi ndani ya Serikali kuuangalia kwa jicho la tatu mradi huo kwa sababu ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza (SGR) hautakuwa na maana kama hautaungwanishwa na bandari ya kisasa.
Kwa mujibu wa Ndugai, bandari ya Bagamoyo itakuwa kubwa na ya kisasa Afrika Mashariki na inaweza kuhudumia nchi nyingi za kusini mwa Afrika.
Januari 8, 2016, Aliyewahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema ujenzi wa bandari ya Bagamoyo utasubiri hadi kukamilika kwa uongezaji wa kina cha maji katika Bandari ya Dar es Salaam na uboreshaji wa Bandari ya Mtwara.
Lakini siku chache zilizopita Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) January Makamba imesitisha mazungumzo na wawekezaji katika bandari ya Bagamoyo, mradi ambao ungegharimu takriban Sh 23 trilioni.
Wawekezaji katika mradi huo walikuwa ni kampuni ya China Merchant Holdings International Limited (CMHI) na State General Reserve Fund (SFRF) ya Oman.