Bunge lamthibitisha Dk Mpango kuwa Makamu wa Rais Tanzania
Wabunge wa Bunge la Tanzania wamemthibitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais kwa kura 363 walizopiga leo Machi 30 Bungeni jijini Dodoma huku kukiwa hakuna kura ya hapana.
- Amethibitishwa baada ya kupigiwa kura na Wabunge 363 ambapo wote wamesema ndiyo na hakuna kura hata moja iliyoharibika.
Dar es Salaam. Wabunge wa Bunge la Tanzania wamemthibitisha Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais kwa kura 363 walizopiga leo Machi 30 Bungeni jijini Dodoma huku kukiwa hakuna kura ya hapana.
Kwa kura hizo ambazo ni sawa na asilimia ya kura zote zilizopigwa na Wabunge, Dk Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango tangu Hayati Rais John Magufuli ashike madaraka mwishoni mwaka 2015 ni rasmi sasa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Kwa kura hizo ambazo ni sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa na Wabunge, Dk Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango tangu Hayati Rais John Magufuli ashike madaraka mwishoni mwaka 2015 ni rasmi sasa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Dk Mpango atafanya kazi kwa karibu na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania Machi 19 mwaka huu baada ya Dk Magufuli kufariki dunia Machi 17 kutokana na maradhi ya moyo.
Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa, Spika Job Ndugai amesema Wabunge waliopiga kura kumthibitisha Dk Mpango kuwa makamu wa rais ni 363 ambapo wote wamempa kura za ndiyo na hivyo hakuna kura iliyoharibika.
“Jumla ya kula zote ziliongezeka, Wabunge wakawa wakiingia, mwisho tukawa Wabunge humu ndani 363, hakuna kura iliyoharibika hata moja. Kwa hiyo idadi ya kura halali ni 363.
“Naomba kutangazia Bunge hili na nchi kwa ujumla kwamba kura za hapana hakuna hata moja, kura zote 363 ni kura za ndiyo, kwa hiyo amepata asilimia 100 ya kura zote,” amesema Spika Ndigai.
Kwa kura hizo, sasa ni rasmi Dk Mpango ni Makamu wa Rais wa Tanzania.
Baada ya kushika nafasi hiyo, Dk Mpango analazimika kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma na ambapo uchaguzi utatangazwa tena ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
Soma zaidi:
Kibarua alichonacho Dk Mpango
Dk Mpango ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) amesema kazi yake kubwa atakayofanya katika nafasi ya makamu wa rais ni kuhakuhakikisha ndoto ya Watanzania ya kuondokana na umasikini inatimia.
“Wanataka SGR yao ikamilike, wanataka bwawa la Mwalimu Nyerere likamilike, wanataka barabara husuan za vijijini zikamailike, wanataka huduma za afya ziwe bora zaidi, wanataka maji, wanataka usalama waendelee kufanya shughuli zao. Hawataki rushwa,” amesema Dk Mpango kuwa atayasimamia hayo yote.
Amesema pale atakapotakiwa kusimamia maslai na rasilimali za umma, utamsaidia Rais Samia kuhakikisha kuwa wanakwenda sawasawa.
“Mniombee kwa mwenyezi Mungu, naomba sana, kila mtu kwa dini yake, dhamana hii ni kubwa sana, umaskini katika nchi yetu ni mkubwa sana. Bado tuna zaidi ya watu milioni 14 wanaishi chini ya kiwango cha umaskini, kiwango hakikubaliki,” amesema muda mfupi kabla ya kutangazwa kwa kura za Wabunge zilizothibitisha jina lake.
Dk Mpango amesema licha ya kuwa yeye ni mcha Mungu na mpole, hatokuwa mpole kwa wanaokula rushwa na watakaotumia fedha za umma hovyo na atasimama imara kutetea maslai ya umma.
Aidha, ametoa shukrani kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Wabunge kwa ujumla akiwasisitiza kuendelea kuishi katika maadili ya uongozi na kufuata misingi ya Katiba ya Tanzania.
“Naendelea kuwasihi waheshimiwa Wabunge, pamoja na kutunga sheria mzisimamie bila uoga, kazi hizi ambazo ziko kwenye Katiba lakini hizi ni kazi ambazo mmepewa na mwenyezi Mungu. Mzifanye kwa uaminifu kabisa,” amesema Dk Mpango.
Dk Mpango katika moja ya shughuli zake akiwa bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha nyuma. Picha| Mtandao.
Wabunge wamuelezea Dk Mpango
Kabla ya Dk Mpango kuthibitishwa kuwa makamu wa rais, baadhi ya Wabunge na Mawaziri walipata fursa ya kuelezea utendaji wake na jinsi ambavyo wanafikiri ni chaguo sahihi la Rais Samia.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amemuelezea Dk Mpango kama mtu ambaye ana uchungu na Taifa lake na mwenye tamaa ya kuisongesha Tanzania mbele.
“Ni watu wachache sana ambao wanadumu katika nafasi ya Waziri wa Fedha kwa miaka mitano. Kwenye masuala ambayo mtu anataka kuchezea chezea rasilimali za nchi hii, hana urafiki hata kidogo na huwa hacheki,” amesema Prof Ndalichako.
Baadhi ya Wabunge wamesema Dk Mpango ana sifa zote kuwa makamu wa Rais kwa sababu ni msikivu, mnyenyekevu na anayependa nchi yake.
“Phillip Mpango amejaliwa unyenyekevu usiokuwa wa kawaida. Phillip Mpango amejaliwa upole lakini uthabiti. Phillip Mpango amejaliwa kauli ambayo haibadiliki,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi bungeni.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi amesema Dk Mpango ni kati ya watu walioaminiwa na Hayati Dk Magufuli kwa kumlea kiuongozi.
Amesema ana uzoefu wa muda mrefu na kiongozi ambaye anajituma tangu zamani na kila alipokabidhiwa kazi.
“Ni mtu anayefaa, anayestahili na ana uwezo wa kufanya haya ambayo anapewa leo,” amesema Lukuvi.