October 6, 2024

Bushungwa awaonya wanaopandisha bei ya barakoa

Waziri huyo ameweka wazi kuwa atachukua hatua kwa taasisi hizo ambazo hakuzitaja kwa majina pale zitakapoendelea kuuza kwa bei zinazojipangia.

  • Ni baada ya baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali kuuza barakoa kwa bei ya juu. 
  • Amesema bei elekezi ya barakoa haitakiwi kuzidi Sh1,500.
  • Watakaokaidi kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amezionya taasisi zisizo za kiserikali (NGO) zilizopewa kibali cha kutengeneza barakoa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Corona kuacha kuuza barakoa kwa bei ya juu ili kujinufaisha.

Bashungwa katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili27, 2020) amesema baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikiuza barakoa hizo kwa bei ya Sh2,500 na Sh3,000 ambayo baadhi ya Watanzania hawawezi kuimudu. 

“Wamekuwa wakitoa masharti kupitia mitandao ya kijamii kuwa hawauzi barakoa chini ya bei hiyo,” amesema Bashungwa. 

Waziri huyo ameweka wazi kuwa atachukua hatua kwa taasisi hizo ambazo hakuzitaja kwa majina pale zitakapoendelea kuuza kwa bei zinazojipangia.

Waziri huyo ametoa onyo akiwa mkoani Arusha alipotembelea Viwanda vya kuzalisha nguo vya Sunflug na A to Z kuangalia hali ya uzalishaji wa barakoa katika viwanda hivyo.


Zinazohusiana


Aidha, amevitaka Viwanda hivyo kuendelea kuzalisha kwa wingi ili wananchi walio wengi wa vijijini waweze kupata vifaa hivyo vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona.

Kiwanda cha Sunflug kina uwezo wa kuzalisha barakoa 25,000 kwa siku huku cha A-Z kina uwezo wa kuzalisha barakoa 15,000 kwa siku.