CAG abaini taasisi tisa zilizofanya malipo ya mamilioni bila kuidhinishwa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amebaini taasisi tisa za Serikali ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria zilifanya jumla ya malipo ya Sh719.5 milioni bila kuidhinishwa na watu waliopewa mamlaka, jambo linaloweza kuwa chanz
- Malipo ambayo hayajaidhinishwa yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Sh188 milioni mwaka 2017/2018 mpaka Sh719 milioni.
- Taasisi hizo tisa za Serikali ziliidhinisha malipo ya Sh719.5 milioni bila kuidhinishwa.
- CAG asema jambo hilo ni ishara ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amebaini taasisi tisa za Serikali ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria zilifanya jumla ya malipo ya Sh719.5 milioni bila kuidhinishwa na watu waliopewa mamlaka, jambo linaloweza kuwa chanzo cha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kuhusu Serikali Kuu iliyotolewa jana (Aprili 6, 2020), CAG Kichere amesema Kanuni ya 88(1) ya Kanuni za fedha za Umma ya mwaka 2001 inamtaka Afisa Masuuli au mtu aliyeidhinishwa kusaini hati zote za malipo kabla malipo hayajafanyika.
“Lakini kinyume chake, nimebaini kuwa taasisi nane zililipa Sh719.5 milioni bila kuidhinishwa,” amesema CAG katika ripoti hiyo.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo ilifanya malipo ya Sh536.8 milioni bila kuidhinishwa, kiasi ambacho ni kikubwa zaidi au sawa na asilimia 74.6 ya malipo yote ya taasisi tisa ambazo zimetajwa na CAG.
Taasisi zingine ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo ilifanya malipo ya Sh40.7 milioni, Tume ya Huduma ya Walimu (Sh15.6 milioni), Wizara ya Katiba na Mambo ya Sheria (Sh36.1milioni), Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (Sh92.2 milioni) na Sekretarieti ya Mkoa Mara iliyolipa Sh25.4 milioni bila kuidhinishwa.
Tume ya Taifa katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu (UNESCO) iliidhinisha malipo ya Sh24.1 milioni, Mahakama ya Tanzania (Sh10.5 milioni) na Sh28.8 milioni yaliidhinishwa na Sekretarieti ya Mkoa Dodoma.
“Ni mtizamo wangu kuwa malipo ambayo hayajaidhinishwa yanaweza kuwa chanzo cha matumizi mabaya ya fedha za umma na Wafanyakazi wasio waaminifu wanaweza kutumia mianya hii kufanya malipo hewa bila menejimenti kujua,” amesema CAG Kichere.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, malipo ambayo hayajaidhinishwa yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Sh188 milioni mwaka 2017/2018 mpaka Sh719 milioni ikiwa ni ishara kuwa hakuna jitihada za dhati zilizofanyika kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani juu ya usimamizi wa matumizi.
Amependekeza kwa maafisa masuuli husika kuhakikisha kuwa malipo yote yanaidhinishwa ipasavyo katika hatua zote na mifumo ya udhibiti wa ndani inayohusiana na uidhinishwaji wa malipo inaimarishwa ili kuiepushia Serikali hasara.
Soma zaidi:
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Malipo yaliyolipwa zaidi
Licha ya kubaini malipo yaliyolipwa bila kuadhinishwa, pia CAG amebaini kuwa taasisi sita zililipa zaidi ya kiwango stahiki jumla ya Sh459.2 milioni kwa ajili ya kununua vitu na huduma mbalimbali.
Kanuni ya 87 ya Kanuni za Fedha za Umma ya mwaka 2001 inataka Ofisa anayesaini hati ya malipo kuthibitisha usahihi wa kila maelezo ya malipo, kinyume chake taasisi hizo zilikiuka kanuni hiyo.
“Ni mtazamo wangu kuwa kiasi kilicholipwa zaidi kilisababishwa na udhaifu wa mfumo wa udhibiti wa ndani wa kuchakata malipo na kutofuata mgawanyo wa bajeti kwa kila kifungu cha matumizi,” amesema CAG katika ripoti hiyo.
Taasisi hizo zilizolipa malipo zaidi ni Sekretarieti ya Mkoa Dodoma ililipa kwenda kwa kampuni ya CRJE East Africa Sh7.5 milioni, Sektretarieti (Sh22.7 milioni), Wizara ya Maji (Sh286 milioni) na Sekretarieti ya Mkoa Tanga ambayo ilituma taarifa zisizo sahihi kwa Wizara ya Elimu ili kupata fedha zaidi za mitihani kiasi cha Sh31.6 milioni
Nyingine ni Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Sh13.2 milioni) na Mahakama ya Tanzania ambayo ililipa Sh75.3 milioni.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, kiasi kilicholipwa zaidi kimeongezeka kutoka Sh133.53 milioni mwaka 2017/2018 hadi Sh459.20 milioni mwaka 2018/2019 japo idadi ya taasisi imebaki vilevile.
Kichere amesema hiyo ni ishara kuwa baadhi ya taasisi zilizokaguliwa hazijaweka mifumo thabiti ya udhibiti wa ndani ambao ungeweza kuondoa tatizo la malipo kulipwa zaidi ya kiasi kinachostahili.
“Napendekeza kuwa: maafisa masuuli waimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani katika kuchakata malipo, kuokoa kiasi kilicholipwa zaidi na fedha hizo kutumika kwenye matumizi kama yalivyoidhinishwa kwenye bajeti,” amesema CAG katika ripoti hiyo.