CAG aibua mapya utengenezaji vitambulisho vya Taifa
Abaini uwepo wa kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni ambazo zimeharibika na hazifai kwa matumizi na matumizi yasiyo sahihi ya taarifa za watu waliosajiliwa kwenye kanzidata ya NIDA.
- Abaini uwepo wa kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni ambazo zimeharibika na hazifai kwa matumizi.
- Matumizi yasiyo sahihi ya taarifa za watu waliosajiliwa kwenye kanzidata ya NIDA.
- NIDA iliingia makubaliano ya ruzuku na Mfuko wa Uwezeshaji Sekta ya Fedha (FSDT) wa Sh6.9 bilioni ili kuzalisha Namba za Utambuzi (NIN) takribani milioni 20 lakini haikufanya hivyo.
Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho mamia ya Watanzania wanasubiria vitambulisho vya uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeibaini uwepo wa kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni ambazo zimeharibika na hazifai kwa matumizi ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
CAG Charles Kichere katika ripoti hiyo ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa mwaka 2019/20 amebaini kuwa muda wa mkataba wa mtoa huduma wa kadi hizo zenye kasoro ulikuwa umeisha tokea miaka mitatu nyuma (Machi 14, 2018), ikiwa ni moja ya kasoro za kitendaji zilibainishwa kutoka katika taasisi hiyo.
Kadi hizo zilizoharibika iwapo zingetumika vizuri zingesaidia Watanzania wengi waliosajiliwa na kupewa namba za utambulisho wa kitaifa (NIN) kupata vitambulisho vyao.
“Licha ya menejimenti ya NIDA kueleza kuwa imetuma barua kwenda kwa mkandarasi (IRIS) ili afanye usuluhisho wa kadi zilizoonekana na matatizo na kubadilisha na kadi mpya, ni maoni yangu kuwa, kuna hatari ya NIDA kupata hasara ikiwa IRIS atashindwa kubadilisha kadi hizo ambazo hazifai kutokana na kukosekana kwa mkataba halali kati ya NIDA na M/s IRIS Corporation Berhad,” imeeleza sehemu ya ripoti ya CAG iliyotolewa Aprili 8, 2021.
Mnamo Aprili 21, 2011, NIDA iliingia kwenye mkataba na kampuni ya IRIS Corporation Berhad ya Malaysia kwa ununuzi wa bidhaa na vifaa vya utekelezaji wa mfumo wa kadi za vitambulisho vya Taifa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 149.9 sawa na Sh347.7 bilioni.
Katika mkataba huo kulikuwa na makubaliano ya kusambaza kadi milioni 25 mpaka kipindi cha ukaguzi, Novemba 2020 ambapo CAG alibaini kuwa msambazaji aliwasilisha kadi milioni 13.7 tu.
“Aidha, uchambuzi wangu ulibaini kwamba, kati ya kadi zilizowasilishwa, NIDA imetumia kadi milioni 6.2 kutengeneza vitambulisho vya Taifa na kubakiza kadi milioni 5.1 zikiwa hazijatumika.
“Hata hivyo, nimebaini kuwa kati ya kadi milioni 5.1 zilizobakia, ni kadi milioni 4.6 tu ndizo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye bohari, huku kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni zikiwa zimeharibika na hazifai kwenye matumizi ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa,” inasomeka sehemu ya ripoti ya CAG.
#CAG: Ukaguzi wangu ulibaini kuwa NIDA ilikuwa na kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni ambazo zimeharibika na hazifai kwa matumizi ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
Muda wa mkataba wa mtoa huduma wa kadi hizo zenye kasoro ulikuwa umeisha tokea miaka mitatu nyuma. pic.twitter.com/DazJ7qIYP2
— Nukta Tanzania (@NuktaTanzania) April 9, 2021
CAG amependekeza NIDA kuboresha udhibiti wa ndani juu ya usimamizi wa kadi za kutengenezea vitambulisho vya taifa na kuhakikisha kuwa M/s IRIS Corporation Berhad inatimiza ahadi ya kufanya usuluhishi wa kadi ambazo hazifai na kubadilisha na kadi mpya.
NIDA yashindwa kuzalisha namba za utambuzi
CAG Kichere katika ripoti yake hiyo anaeleza kuwa alibaini kuwa NIDA iliingia makubaliano ya ruzuku na Mfuko wa Uwezeshaji Sekta ya Fedha (FSDT) wa jumla ya Dola za Marekani milioni 3 (Sh6.9 bilioni) ili kuzalisha Namba za Utambuzi (NIN) takribani milioni 20 kwa kutumia taarifa za wapiga kura za mwaka 2015.
“Hata hivyo, nilibaini kuwa NIDA ilitumia jumla ya Dola za Marekani milioni 1.2 (Sh2.6 bilioni) kati ya Dola za Marekani milioni 3 iliyoahidi. Hata hivyo, hakukuwa na Namba za Utambuzi (NIN) zozote zilizozalishwa na NIDA,” amesema CAG.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli ataja sababu za kuwang’oa Kichere TRA, Kakunda wizara ya viwanda
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
Matumizi yasiyo sahihi ya taarifa za watu
Katika kipindi hicho cha 2019/20, CAG alibaini kuwa NIDA iliruhusu taasisi 40 kupata taarifa za watu waliosajiliwa kwenye kanzidata ya NIDA bila kufanya malipo kwa mamlaka hiyo kama sheria inavyotaka.
“Ukaguzi wangu wa ziada wa mfumo, ulibaini taasisi hizo zilibonyeza kitufe kupata taarifa mara milioni 89.2 ambapo NIDA angeweza kukusanya mapato ya Sh44.6 bilioni,” amesema CAG Kichere.
Kutokana na changamoto hiyo, CAG amesema “maoni yangu kuwa, Serikali inakosa fedha ambazo zingesaidia NIDA kugharamia shughuli zake na kupunguza utegemezi kwa serikali.”