CAG aibua mazito malipo Benki Kuu ya Tanzania
CAG Charles Kichere katika ukaguzi wake amebaini mapungufu ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo bandari.
- Mapungufu hayo ni ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika taasisi mbalimbali za Serikali.
- Baadhi ya taasisi zilifanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa.
- Mapungufu mengine ni kuwepo kwa miradi ambayo haikupangwa na hivyo kufanya malipo nje ya bajeti.
Mwanza. Ripoti maalum ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imebaini kuwa fedha zilizotolewa katika benki hiyo kuanzia Januari hadi Machi 2021 zilifuata taratibu zote, isipokuwa baadhi ya malipo yalikuwa na mapungufu.
Hayo yamebainika leo Julai 1, 202021 jijini Dodoma baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupokea taarifa ya ukaguzi maalum kutoka kwa CAG inayohusu matumizi ya fedha zilizotolewa BoT kuanzia Januari hadi Machi 2021.
Ripoti hiyo ni matokeo ya agizo la Rais Samia alilolitoa Machi 28 mwaka huu ambapo alimtaka CAG kwa kushirikiana na Gavana wa benki kuu kufuatilia fedha zote zilizotoka kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili zionekane kama zimefanya kile kilichokusudiwa au la.
Sambamba na hilo aliagiza Deusdedit Kakoko, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) asimamishwe kazi mara moja kupisha uchunguzi wa ubadhirifu dhidi ya taasisi hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Rais Samia aliyekuwa akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mwaka 2019/20 Ikulu jijini Dodoma alisema imebainika uwepo wa ubadhirifu wa Sh3.6 bilioni katika taasisi hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea Taarifa ya Ukaguzi Maalum inayohusu matumizi ya Fedha zilizotolewa BOT kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu, kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere Jijini Dodoma leo tarehe 01 Julai, 2021.Picha|Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, CAG Charles Kichere katika ukaguzi wake amebaini mapungufu ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika taasisi mbalimbali za Serikali.
“Mapungufu hayo ni pamoja na baadhi ya taasisi za serikali kama vile Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), zilifanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Jaffar Haniu.
CAG Kichere amesema mapungufu mengine ni pamoja na baadhi ya makandarasi waliotoa huduma walicheleweshewa malipo yao hali inayosababisha madeni ya makandarasi kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali.
“Mapungufu mengine ni kuwepo kwa miradi ambayo haikupangwa na hivyo kufanya malipo nje ya bajeti,” amesema CAG katika taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Rais Samia amepokea taarifa ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022 kutoka kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa.
Dk Chuwa amesema Sensa ya mwaka 2022 itatumia teknolojia ya kisasa ya kidigitali chini ya mfumo uliopo wa Serikali katika ngazi zote za utawala kwa pande zote za Muungano.
Amesema Sensa ya majaribio itafanyikia mwezi Agosti mwaka huu katika Mikoa saba kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.