October 7, 2024

CAG ataja taasisi 14 zilizofanya malipo bila kudai risiti za EFD

Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambazo zilifanya malipo ya Sh7.95 bila kudai stakabadhi za kieletroniki.

Serikali imeshauriwa kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya hiari ya mashine za EFD zitakazochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali. Picha!Mtandao.


  • Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na  Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambazo zilifanya malipo ya Sh7.95 bila kudai stakabadhi za kieletroniki.
  • Lakini idadi ya taasisi za Serikali zinazofanya malipo bila kudai risiti za EFD imepungua kwa asilimia 26.

Dar es Salaam. Wakati watanzania wakiendelea kujadili ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu ya mwaka 2017/2018, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Professa Mussa Juma Assad amesema taasisi za Serikali 14 zilifanya malipo ya Sh7.95 bilioni bila kudai stakabadhi za kielektroniki (EFD).

Sheria ya Usimamizi wa kodi ya Mwaka 2017 Kifungu 36 inamtaka kila mtu anayetoa huduma kutoa stakabadhi kwa kutumia kifaa cha kielektroniki (Electronic Fiscal Device)

Katika ripoti yake ya ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu ya mwaka 2017/2018 amesema taasisi za Serikali 14 zilifanya malipo ya kiasi cha Sh7.95 kudai stakabadhi za kieletroniki ambapo ni kinyume na Kanuni namba 28(1) ya Kanuni za Sheria ya Kodi ya Mapato (Mashine za Stakabadhi za Kielektroniki) ya mwaka 2012. 

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ambayo ilifanya malipo ya Sh131.96 milioni na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambao uliongoza kwa malipo makubwa yasiyo na risiti za EFD ya Sh6.57 bilioni.

Taasisi nyingine ni Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Prisons Corporation, SUMA Agriculture and industrial segment, Taasisi ya Uongozi Institute na Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji ambao ulifanya malipo ya Sh24.59 milioni.

Hata hivyo, idadi ya taasisi za Serikali zinazofanya malipo bila kudai risiti za EFD imepungua kutoka 19 hadi 14, kutokana na jitihada za Serikali kutoa elimu na kuhimiza wafanyabiashara na taasisi kutumia mfumo huo wa kielektroniki ili kuepousha upotevu wa mapato.

“Mwaka 2016/2017 aliripoti kiasi cha malipo ya Shilingi 42,407,098,471 kutoka katika Wakala, Bodi za Mabonde ya Maji, na Taasisi nyingine za serikali yaliyofanyika bila kudai risiti za kielektroniki (EFD),” 

“Kwa mwaka huu wa 2017/2018 tatizo hili la kutokudai risiti limepungua kwa kiasi kikubwa katika Taasisi za Umma na kufikia kiasi cha Sh. 7,956,320,106.61, sawa na asilimia 81 ikilinganishwa na kiasi cha Sh. 42,407,098,471 mwaka uliopita,” inasomeka sehemu ya ripoti ya CAG. 


Soma zaidi:


Amebainisha kuwa taasisi zisizochukua stakabadhi za kieletroniki zimepungua kwa asilimia 26, wakati kiasi cha malipo kisichokuwa na stakabadhi za kielektroniki kimepungua kwa asilimia 81 ikilinganishwa na kiasi cha mwaka 2016/2017.

Serikali imeshauriwa kuendelea kutoa elimu juu ya utekelezaji wa hiari wa Kanuni na Sheria ya Kodi ya Mapato za mwaka 2012 kuhusu matumizi ya hiari ya mashine za EFD zitakazochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali kama kila manunuzi ya Serikali yataambatana na stakabadhi za kielektroniki.