October 6, 2024

CAG Kichere alivyojipanga kuendeleza kazi ya Prof Assad

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Charles Kichere amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ambayo yameachwa na CAG aliyemaliza muda wake, Prof Mussa Assad kwani Ofisi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Watanzania.

  • Amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ambayo yameachwa na CAG aliyemaliza muda wake, Prof Mussa Assad.
  • Amesema atahakikisha kuwa analinda kodi ya Watanzania ili iweze kunufaisha makundi yote.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Charles Kichere amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ambayo yameachwa na CAG aliyemaliza muda wake, Prof Mussa Assad kwani Ofisi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Watanzania.

Akizungumza katika makabidhiano ya ofisi leo (Novemba 5, 2019) jijini Dar es Salaam, Kichere amesema kuwa Ofisi ya CAG ni nguzo muhimu kwa Watanzania kwani ndiyo ofisi inayolinda na kuangalia matumizi sahihi ya kodi yao wanayolipa kila siku.

“Niwaahidi kwanza tutaendelea kufanya kazi hii ambayo ambayo imefanywa na Prof Assad na timu yake, nitahakikisha kushirikiana na wafanyakazi wa Ofisi hii kwa umakini mkubwa sana.

Tutafanya kazi hii kwa kuzingatia weledi, uadilifu kama alivyosema Profesa. CAG huwa siye anayefanya kazi, CAG anawajibika kwa kusaini ripoti, lakini ripoti inaanzia chini kwa wafanyakazi,” amesema CAG Kichere.  

Kichere amesema kuwa katika kutekeleza majukumu hayo mapya atahakikisha kuwa atalinda kodi ya Watanzania ili iweze kunufaisha makundi yote ikiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wafanyakazi. 

“Nataka kufanya kazi kulinda maslahi ya Watanzania, nimefanya kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) najua ugumu wa kukusanya kodi na kupata mapato, kwa hiyo nitahakikisha kuwa nailinda kodi ya wananchi kwa wivu mkubwa sana”, amesisitiza Kichere.


Zinazohusiana:   


Kichere aliteuliwa kuwa CAG Novemba 3 akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Mussa Assad ambaye anamaliza muda wake wa miaka mitano.

Kabla ya Kichere kuteuliwa kuwa CAG alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na kabla ya hapo alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nafasi yake ilichukuliwa na  Edwin Mhede. 

CAG aliyemaliza muda wake Prof Mussa Assad amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Ofisi hiyo licha ya kustaafu lakini atakuwepo kwa wakati ambao atahitajika kutoa msaada kutokana na uzoefu na ujuzi aliopata kwa muda wa miaka mitano akiwa anatumikia ofisi hiyo.

“Nataka nikuambie CAG mpya ukihitaji msaada wa kitu chochote kiwe cha binafsi au cha kiofisi, ujuzi na uzoefu wa kazi hii niko tayari kushirikiana na wewe na utapata msaada huo kwa haraka”, Alisema Prof. Assad.