CAG Profesa Assad alivyoteka mitandao ya kijamii
Baadhi ya wachangiaji katika ukurasa wa Twitter wamemsifu kwa umahiri wake wa kusimamia Katiba na kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2017/2018 licha ya Bunge kukataa kufanya naye kazi.
- Baadhi ya wachangiaji katika ukurasa wa Twitter wamemsifu kwa umahiri wake wa kusimamia Katiba na kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya mwaka 2017/2018 licha ya Bunge kukataa kufanya naye kazi.
- Wengine wamemtaka kuendelea kusimamia Katiba katika majukumu yake ili kuhakikisha kodi za watanzania zinatumika vizuri kutekeleza miradi ya maendeleo.
- Serikali nayo imeshauriwa kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti hiyo ili kuongeza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.
Dar es Salaam. Imepita siku moja tangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Professa Mussa Juma Assad atoe kwa umma ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 huku ripoti hiyo ikiibua maoni mseto kwenye mitandao ya kijamii kutokana na mambo mbalimbali ya uwajibikaji aliyoyaibua.
Katika mtandao wa Twitter watu wa kada tofauti wanaendelea kutoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo na jinsi ambavyo inaibua changamoto za utendaji na usimamizi wa rasilimali za umma nchini.
Ripoti hiyo ilitolewa jana (Aprili 10,2019) Jijini Dodoma na kuwasilishwa bungeni mapema asubuhi kwa ajili kujadiliwa na wabunge.
Wakati Prof Assad akizungumza na Wanahabari jijini humo aliibua mambo mbalimbali yaliyopo kwenye ripoti yake ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kununua gari jipya aina ya Nisan Patrol kwa Sh147.5 milioni lakini lililisajiliwa kwa jina la mwanachama badala ya Bodi ya Wadhamini huku Jeshi la Polisi likilipa Sh600 milioni kwa ajili ya mafunzo ambayo hayakufanyika
Alifafanua zaidi kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilinunua BVR 8,000 lakini mashine 5,000 kati ya hizo zilikuwa haziendani na mfumo uliotakiwa hivyo kuisababisha serikali hasara ya mamilioni ya shilingi. Pia imebainika kuwa Wilaya ya Hanang’ haikuwasilisha vitabu vya fedha na kuna upotevu wa mapato ya Sh. bilioni 1.4 na walilipa fedha kwa wakandarasi kwa kazi ya dharura pasipo kuwapo kwa kazi ya dharura.
Baada ya CAG kuweka wazi ripoti hiyo, mtandao wa Twitter hasa kwa watumiaji wake wa Tanzania ulitekwa na ajenda ya CAG kutokana na madudu yaliyoibuliwa ambapo watu wametoa maoni tofauti huku wengi wakimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya.
Nukta inakuletea baadhi ya maoni ya watu yaliyotolewa katika mtandao wa Twitter kuhusu ripoti hiyo:
Amani Mwaipaja ambaye kitaaluma ni Mwanasheria amesema ripoti hiyo haitawaacha salama baadhi ya watendaji serikalini kutokana na ubadhirifu mkubwa uliotokea katika baadhi ya mashirika.
“Nimeipitia ripoti ya CAG kikamilifu, ninachokiona ni kwamba kuna kimbunga kinakuja cha utumbuaji, na kwakuwa siasa ni mchezo, tusubiri matokeo tu, kuna watu wanatumbuliwa muda si mrefu, hayo mengine mnayoyasikia ni sehemu tu ya mchezo. Kumbuka siasa ni mchezo,” ameandika Mwaipaja katika ukurasa wake.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Professa Mussa Juma Assad wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2017/2018 jana Jijini Dodoma.
Julius Massabo anafikiri CAG Prof Assad amesimamia ukweli na amewajibika ipasavyo katika nafasi yake ya ukaguzi wa hesabu za Serikali.
“Yaani Huyu mzee ndio mpenzi wa Mungu maana anajisemea zake ukweli yaani CAG anajua kabisa kwamba atakachokisema Waandishi wanaweza kabisa asiripoti sababu watawala hawapendi ripoti zisizowapendeza. Tunasafari ndefu kwa kweli,” amesema Massabo.
Naye Godfrey Charles Bishanga ameandika ”#Hongera CAG kwa kuishi Ukweli na kukataa Uongo.”
Nabir Omar ambaye ni mtumiaji wa muda mrefu wa Twitter hasa katika mambo yanayohusu maslahi ya Taifa anamuona Prof Assad kama shujaa licha ya bunge kukataa kufanya naye kazi kwa kile ilichodai kuwa lilidhalilishwa kwa kuitwa ‘dhaifu’.
Omar anaandika kuwa, “Bunge kumkataa na kukana ripoti ya CAG inaashiria kwamba wanataka CAG ambaye atakula rushwa na kuruhusu fedha za walipa kodi na wahisani kutumiwa hovyo, Assad ni shujaa ambaye anafanya kazi kwa uweledi na kuendana na jinsi Rais @MagufuliJP anavyopinga ubadhirifu wa fedha za umma.”
Mchangiaji mwingine katika ripoti ya CAG, Frank Fedelis amesema sakata la bunge kumtenga CAG limewaamsha wananchi kuanza kufuatilia kwa ukaribu ripoti yake iliyotolewa mwaka huu na kujua kwa undani kinachoendelea katika ofisi za umma.
Soma zaidi:
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
Wanaharakati nao hawajabaki nyuma
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume ameitumia siku ya jana kuchambua ripoti hiyo kwa undani kwa kuainisha baadhi ya maeneo yenye upungufu katika ukurasa wake wa Twitter yaliyoibuliwa katika ripoti ya CAG.
Hata hivyo, Fatma ameungana na watu wengine kumpongeza CAG kwa ujasiri na busara alizoonyesha wakati akikamilisha kazi yake ya ukaguzi ambayo imewekwa wazi katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
“I love this man (nampenda huyu mtu). Ana ueleo, subra, ujasiri, busara, uzalendo! @bunge_tz mshabadilisha utaratibu bila ya kujua na Job kwa UBABE wake katuletea Utaratibu BORA. Mwakani CAG atasoma Ripoti yake kutoka kwake.” ameandika Fatma.
Naye Mwanaharakati wa haki za kisiasa, Maria Sarungi ambaye anaendesha kampeni ya Change Tanzania amemtaka CAG kutoteteleka na aendelee kusimamia taaluma yake ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Pia alianzisha hashtag ya #IStandWithCAG baada ya bunge kukataa kufanya kazi na CAG ambayo ilipata muitikio mkubwa kwa watumiaji wa Twitter.
#IStandWithCAG
Kwani kuna anayeteseka?
Piga kazi Prof Assad .. shika taaluma yako waache wanasiasa wapige siasa .. umetimiza wajibu wako
Tuko pamoja na wewe 💪🏽#ChangeTanzania
https://t.co/6zsGYFIMmy— Maria Sarungi Tsehai (@MariaSTsehai) April 10, 2019
Wanasiasa nao wametoa neno
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Heri James wakati akihojiwa leo asubuhi katika kipindi cha Globe360 cha runinga ya Clouds amesema CAG ni kioo chetu sisi, anatafsiri kile ambacho tumekifanya katika taasisi za umma na muhimu kuyafanyia kazi mapendekezo aliyoyatoa kwenye ripoti yake
“Mimi nasimama na CAG kwasababu ndiye anayesimamia maslahi yetu,” amesema James ambapo watu wameyatumia maneno yake kwenye mtandao wa Twitter.
Naye mwanachama mpya wa chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa ameandika, “Tunasubiri tuone Serikali ‘inayowajali wanyonge’ ikiwawajibisha waliohusika na ufisadi huu wa zaidi ya Sh800 milioni ndani ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).”
Licha ya CAG kuibua madudu ya mahesabu katika mashirika ya umma na Serikali Kuu ametoa mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha utendaji ikiwemo watendaji kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha wa walipa kodi.
“Msimamo wa kusimamia HAKI ni tabia adimu. Msingi wake unaimarisha tabia ya aina hii katika Nchi na thawabu yake utalipwa na Mungu. Nina furahi sana kwamba wewe bado ni imara ktk Haki. Mimi/Mh Halima Mdee tumesimamishwa Bunge, lakini umekuwa faraja wa adhabu yetu hii,” ameandika Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye yeye pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wameshimamishwa kuhudhulia vikao vya Bunge kwa sababu ya kuunga mkono kauli ya CAG ya kuliita ‘Bunge Dhaifu’
Naye Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) Hussein Bashe katilka ukurasa wake wa Twitter ameandika maneno mafupi yanayosomeka “Kwa hisani ya Masoud Kipanya” yaliyoambatana na picha ya kibonzo cha mchora katuni huyo.