October 7, 2024

Corona ilivyoathiri biashara ya simu Tanzania

Ugonjwa huo umepelekea kulala kwa biashara hiyo kwakuwa wadau wake sasa wamehamia kwenye manunuzi ya mahitaji muhimu.

  • Wafanyabiashara walalamika kukosa wateja na hawawezi tena kuingiza mzigo mpya.
  • Wachambuzi wa biashara wasema watu wameanza kujihami kwa kupunguza manunuzi ya bidhaa hasa zisizo na umuhimu mkubwa.
  • Washauri wafanyabiashara hao kuepuka uwekezaji mkubwa kwenye biashara hiyo hata baada ya Corona kuisha.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya Corona kumeathiri karibu kila sekta duniani; kuanzia utalii, usafirishaji na uzalishaji viwandani. 

Kampuni zinazotengeneza simu duniani nazo hazijabaki salama. Zinakabiliwa na kushuka kwa mauzo kutokana na kupungua kwa usambazaji wa vifaa hivyo vya mawasiliano duniani.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, ugonjwa wa Corona ulifyeka mauzo ya simu janja nchini China kwa asilimia 55 huku kampuni ya Apple ya Marekani ikitangaza kuathirika na kupungua kwa kasi ya uzalishaji wa bidhaa zake.

Kampuni hiyo inayozalisha simu za iPhone na kompyuta za Mac, mnamo Februari ilitangaza kuwa huenda isifikie matarajio yake ya kimapato iliyojiyaweka kutokana na ugonjwa wa Corona hasa baada ya manunuzi ya nchini China kupungua.

Apple imesema, “inapitia marejesho ya taratibu kuliko ilivyotazamia.”

Hata wakati Apple ikipitia hayo, hivi karibuni kampuni ya vifaa vya kielektoniki ya Samsung imesema licha athari za Corona bado ina matazamio kuwa mapato yake yatapanda kwa asilimia tano (kufikia  zaidi ya Sh103.8trilioni) katika robo ya kwanza ya mwaka.

Simu za kampuni hizo zimekuwa zikitumiwa na watu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, lakini kwa kiasi gani janga hilo la dunia linaweza kuathiri biashara hiyo nchini?

Wadau wa biashara hiyo wamesema mbali na kukosekana kwa mzigo mpya kwenye maduka, watu hawanunui bidhaa hiyo. Picha| Tanzania Tech.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya True Maisha Erick Chrispin inayojihusisha na ukufunzi wa kibiashara amesema huenda hata Corona itakapoisha, bado wafanyabiashara wa simu watakuwa na sintofahamu kwenye biashara zao.

Amesema endapo marufuku ya kutembea na usafirishaji wa bidhaa duniani  itakapoisha na usafirishaji utakaporuhusiwa, “usambazaji wa simu utakuwa mkubwa lakini nguvu ya manunuzi kwa Watanzania itakuwa ndogo.”

Chrispin amesema kwa sasa Watanzania wengi wanatumia fedha kwa uangalifu na kupunguza matumizi yasiyo ya ulazima na simu zinaweza kukosa wateja. 

Mdau huyo wa biashara amesema, hali hiyo inaweza kupelekea wafanyabiashara wengi kuishia kuuza bidhaa zao kwa bei ya hasara.

Naye Gabriel Mafie ambaye ni mtafiti wa mambo ya uchumi amesema ugonjwa wa Corona umeharibu mnyororo wa thamani kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo za kielektoniki.

“Mnyororo wa thamani kuanzia kwenye uzalishaji, usafirishaji, usambazaji, uuzaji mpaka inamfikia mlaji wa mwisho mchakato wote huo unavurugwa na mkwamo unaosababishwa na Covid-19,” amesema.

Mafie amesema uharibifu huo umechochewa na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa kuanzia zinapotengenezwa na pia ugumu wa usafiri baina ya nchi na nchi.

Amesema hali hiyo inaweza kusababisha tabia za wanunuzi wa bidhaa kubadilika na kuhamia kwenye bidhaa nyingine za vyakula na zile zinazohitajika zaidi zikiwemo vitakasa mikono na barakoa na hivyo kuacha bidhaa za kielektroniki zikiwemo simu kubaki kuwa bidhaa za ziada.

Simu zimekuwa miongoni mwa vifaa muhimu vya mawasiliano na kutafuta vitu mtandaoni. 

Wadau wameshauri wawekezaji wa biashara hiyo kuepukana na uwekezaji mkubwa. Picha| Rodgers George.

Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga James Sibale ambaye ni mtumiaji mzuri wa simu amesema kwa sasa uhitaji wa simu unashuka kutokana na watu wengi kuchagua kununua vyakula na kuweka ndani kwa hofu ya kuenea kwa Corona.

Hata hivyo, athari hizo tayari zimeanza kuonekana kwa wafanyabiashara wadogo wa simu nchini ambapo wameanza kupoteza wateja na kutishia anguko la biashara zao. 

Mfanyabiashara wa simu na vifaa vya kielektroniki wa Jijini Dar es Salaam Marugu Mohammed amekiri kuwa Corona ni janga na amesema “linamuathiri kila mtu” katika shughu zake za kila siku. 

Mohammed ambaye kwa sasa anaweza akamaliza siku bila kuuza simu amesema ana miezi kadhaa sasa bila kuingiza mzigo mpya kwenye duka lake.

“Wafanyabiashara wadogo tunawategemea wafanyabiashara wakubwa wanaosafiri kwenda nchi mbalimbali kama China na kwingineko. Sasa hivi usafiri hamna hivyo na mizigo ndiyo kama unavyoona. Hamna,” amesema Mohammed huku akionyesha duka lake ambalo kwa sasa halina wateja.


Zinazohusiana


Wafanyabiashara wa simu wanatakiwa kufanya nini?

Sibale amewataka wafanyabiashara wa simu kuendelea kufanya biashara zao kwa tahadhari kubwa ya kujikinga afya zao na zaidi kulinda mitaji yao. 

“Ni wazi kwa sasa soko lao nao linayumba kwa maana kwamba demand ya simu imepungua kwa sababu kununua simu kwa kipindi hiki siyo kipaumbele cha Mtanzania,” amesema.   

Naye Mafie ameshauri wafanyabiashara kuepuka kufanya uwekezaji wa muda mrefu na badala yake kuwa wabunifu kwa kuangazia masoko mengine yakiwemo ya mtandaoni.

Kwa pamoja wadau hao wameshauri umma wa Watanzania kuangazia manunuzi ya bidhaa muhimu na siyo za anasa (Luxurious) hasa katika kipindi hiki cha Corona.