Corona ilivyoathiri shughuli za utalii duniani
Msikiti wa Macca, Mnara wa Eiffel na vivutio vingine vilivyojaza maelfu ya watu kwasiku sasa vinalia upweke.
- Vivutio vya kitalii kuanzia mnara wa Eiffel, Ufaransa hadi migahawa ya Piazza na Navona nchini Italia vimefungwa.
- Hali hiyo inatarajia kusababisha hasara ya matrilioni ya fedha katika sekta ya utalii.
- Virusi vya Corona vimezuia watu kusafiri na kukusanyika katika matukio mbalimbali.
Dar es Salaam. Ni ajabu vile ugonjwa wa Corona umeathiri shughuli za kitalii duniani. Kutoka vivutio vilivyokuwa vinajaza watu hadi kufikia kutokuwa na watu kabisa vivutio kubaki vitupu. Inaweza kukuacha ukiwaza ni nini kitatokea siku za usoni.
Kuanzia Msikiti wa Macca ambao unarekodi ya kukusanya waumini wa Kiislamu kutoka takribani kila kona ya dunia hadi Western Wall ya Jerusalem ambayo ni sehemu muhimu kwa dhehebu la waumini la Wayahudi “Judaism” kote utaona mtu mmoja mmoja nao siyo wakaaji bali wapitaji.
Hiyo ni chumvi tu, ambayo Corona imesababisha kwenye utalii, picha kamili hii hapa;
Kama umekuwa ukifuatilia Piramidi ya vioo ya Louvre iliyopo Ufaransa na vivutio vingine nchini humo vikiwemo mnara wa Eiffel na Holi la vioo la Chateau de Versailles utakuwa unafahamu wingi wa watu wanaotembelea vivutio hivyo. Lakini sasa hali imebadilika.
Mwaka 2019, Piramidi ya Louvre ilijizolea jumla ya watalii milioni 9.6 ikiwa ni kwa mujibu wa redio ya kimataifa ya Ufaransa (RFI) ambayo ni sawa na watu 36,301 kwa siku moja.
Kwa sasa hakuna watalii tena katika eneo hilo maana mamlaka zimefunga na watu haruhusiwi kutembelea mpka virusi vya Corona vitakapomalizwa.
Awali watalii 36,301 walitembelea piramidi hii kwa siku lakini kwa sasa hali ni tofauti. Picha| Reddit.
Kwa nchi ya Italia mambo siyo mambo kwani mbali na sehemu za kitalii hata mitaa haina watu kiasi cha kuusikia mwangwi wako endapo utapiga Yowe. Watu wamejifungia nyumbani.
Vivutio vya migahawa ya Piazza Navona, ngazi za Spanish Steps, Trevi Fountain na Roman Forum vyote vikiwa kwenye mji wa Roma nchini humo viko kimya. Huenda vinapitia anguko kubwa la kitalii kuwahi kutokea tangu vita vya pili vya dunia vimalizike.
Migahawa ya Piazza Navona ni kati ya sehemu zinazokuwa na watu wengi siku za kawaida lakini kutokana na watu wengi kujitenga na kukaa majumbani kwao, migahawa hiyo haina watu tena.
Utalii wa boti wa Wat Arun wa huko Bangkok, Thailand ni kati ya sehemu zilizopata pigo la ugonjwa wa Corona kwani boti nyingi zimebaki zikiyumba yumba kwenye sehemu ya maegesho zikiwa hazina watalii.
Wat Arun ambayo hupata watalii wengi kutoka China huenda ikaandika historia mbaya mwaka huu baada ya Corona kufanya maafa hayo kwa kuzuia mikusanyiko ya watu wengi.
Kwa mujibu wa Baraza la Utalii Duniani (UNWTO), janga la ugonjwa wa Corona linatarajiwa kusababisha hasara ya Sh50.2 trilioni hasa ikizingatiwa kuwa hadi sasa, hakuna tiba wala chanjo ya ugonjwa huo.
Zinazohusiana
- Hifadhi za Taifa unazoweza kuzitembelea kidijitali kwenye simu yako
- Ifahamu ‘paradiso’ ya baharini iliyopo Kaskazini mwa Tanzania
- Kisiwa cha Mafia: Pepo kwa ajili ya wapendanao
Nalo Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi sasa umesababisha vifo vya watu 14,510 huku watu 332,930 wakithibitika kuwa na maambukizi hadi jana Machi 23, 2020.
Katika nchi za Afrika nako utalii umeathirika, baadhi ya nchi kama Kenya, Uganda na Rwanda zimesitisha kupokea wageni ili kujikina na ugonjwa huo.
Hiyo ni sawa na kusema shughuli nyingi za utalii katika bara la ulaya, Asia na hata Africa zitasimama na kuathiri mapato ya sekta hiyo muhimu kukuza uchumi wa Taifa.