Corona ilivyoshusha mapato sekta ya utalii Tanzania
Mapato yatokanayo na sekta ya utalii Tanzania yameshuka zaidi ya mara tatu ndani ya mwaka mmoja kutokana na kupungua kwa idadi ya watalii wa kimataifa kulikosababishwa na janga la Corona.
- Yamepungua hadi Sh1.6 trilioni mwaka 2020 kutoka Sh6.1 trilioni mwaka 2019.
- Kupungua huko kumesababishwa na janga la Corona na kupungua kwa watalii wa kimataifa.
- Serikali yasema licha ya Corona, watalii wanaendelea “kumiminika” Tanzania.
Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na sekta ya utalii Tanzania yameshuka zaidi ya mara tatu ndani ya mwaka mmoja kutokana na kupungua kwa idadi ya watalii wa kimataifa kulikosababishwa na janga la Corona linaloendelea kuitesa dunia kwa sasa.
Mapato hayo yameshuka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 (Sh6.1 trilioni) yaliyopatikana mwaka 2019 hadi Dola za Marekani milioni 714.5 (Sh1.6 trilioni) mwaka 2020.
Hiyo ni sawa upungufu wa Sh4.5 trilioni ambazo zingepatikana zingesaidia kuikuza sekta hiyo na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla katika taifa hilo la Afrika Mashariki linalojulikana kwa umaarufu wa vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro na hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Hata hivyo, mapato ya sekta ya utalii yamekuwa yakiongezeka kila mwaka isipokuwa mwaka jana kutokana na athari za janga la Corona.
Kushuka kwa mapato hayo ya utalii kumechangia kwa sehemu kubwa na kupungua kwa idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Tanzania.
Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2021/22, idadi ya watalii wa kimataifa waliotembelea Tanzania walikuwa 620,867.
Idadi hiyo imepungua kutoka watalii milioni 1.5 walioingia nchini mwaka 2019 sawa na anguko la asilimia 59.3 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Kupungua kwa idadi ya watalii walioingia Tanzania mwaka jana kulisababishwa na COVID-19 ambapo nchi nyingi zilizuia usafiri wa anga na raia wake kusafiri katika maeneo mbalimbali duniani ili kujikinga na janga hilo.
Zinazohusiana:
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amesema kwa kuzingatia mwenendo wa ukuaji wa sekta ya utalii nchini, katika mwaka 2020, wizara ilitarajia kupokea watalii milioni 1.8.
“Makisio hayo yalikuwa ni kabla ya kutokea kwa janga la COVID-19. Baada ya mlipuko wa COVID-19, wizara ilifanya tathmini ya athari za ugonjwa huo katika sekta ya utalii na kuweka makisio mapya ya jumla ya watalii 437,000 yaliyozingatia hali halisi ya uwepo wa COVID-19,” amesema Dk Ndumbaro.
Baada ya makisio hayo, Tanzania ilifanikiwa kupata watalii 620,867 wa kimataifa na kuvuka lengo lililowekwa.
“Tanzania imeendelea kupokea watalii licha ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19,” amesema Dk Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini.
Licha ya changamoto hizo za mapato, Tanzania pia imeendelea kufungua masoko mapya ya utalii ikiwemo nchi za Urusi, Poland na Ukraine na kuorodheshwa na nchi ya Urusi kuwa miongoni mwa nchi tatu duniani ambazo ni salama kwa wananchi wake kutembelea.
Utalii ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa fedha za kigeni Tanzania sanjari na madini hususan dhahabu.