November 24, 2024

Corona inasababishwa na virusi siyo bakteria

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa Corona inasababishwa na kirusi aina ya COVID-19 na siyo bakteria kama inavyodhaniwa na kuelezwa na baadhi ya watu mtandaoni.

  • Corona ni jamii ya virusi aina ya COVID-19 na siyo bakteria. 
  • Lakini baadhi ya watu ambao wanapata maradhi ya COVID-19 wanaweza kupata shida ya maambukizi ya bakteria.
  • Ukipata Corona nenda kituo cha afya ufanyiwe uchunguzi.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa virusi vya Corona ni zaidi ya ugonjwa unaothiri afya za watu kwa sasa baada ya kuwa ni chanzo cha uzalishaji wa habari za uzushi ambazo zina madhara zaidi kwa uchumi na maisha ya watu. 

Kwa sasa, mkanganyiko ambao umekuwa ukitokea hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ni kuhusu kisababishi cha ugonjwa wa Corona.

Wapo wanaosema unasababishwa na virusi na wengine wanadai ni bakteria. Licha ya kuwepo elimu ya muda mrefu kuhusu corona, bado kuna maudhui potofu kuhusu chanzo cha maradhi yanajipenyeza. Je, nani yuko sahihi?


Zinazohusiana:


Ukweli uko hivi

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa Corona inasababishwa na kirusi aina ya COVID-19 na siyo bakteria kama inavyodhaniwa na kuelezwa na baadhi ya watu mtandaoni. 

“Kirusi kinachosababisha COVID-19 ni familia ya virusi vinavyojulikana kama “Coronaviridae”, imesema WHO.

WHO imeeleza kuwa dawa za kuzuia au kuua bakteria (Antibiotics) haziwezi kufanya kazi dhidi ya virusi hivyo kwa sababu matibabu yake hutegemea dalili za mgonjwa. 

Hata hivyo, baadhi ya watu ambao wanapata maradhi ya COVID-19 wanaweza kupata shida ya maambukizi ya bakteria.

“Kwa kesi hii, dawa ya antibiotics zinaweza kupendekezwa na mtoaji huduma za afya,” imesema WHO. 

 Shirika hilo limeendelea kusisitiza kuwa mpaka sasa hakuna dawa iliyothibitishwa kutibu COVID-19.

Kama umepata dalili za ugonjwa huo nenda katika kituo cha afya ili upate matibabu stahiki.