Corona yachangia idadi ya wanaofanyia kazi nyumbani kupaa
Kutokana na janga la COVID-19, takriban watu milioni 260 walikuwa wanafanyia kazi nyumbani duniani kote wakiwakilisha asilimia 7.9 ya ajira zote duniani.
- Takriban watu milioni 260 walikuwa wanafanyia kazi nyumbani duniani kote wakiwakilisha asilimia 7.9 ya ajira zote duniani.
- ILO yasema kufanyia kazi nyumbani kuna changamoto nyingi.
- Yataka hatua za dharura kuboresha maslahi ya watu wanaofanyia kazi nyumbani.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) imeeleza kuwa mlipuko wa janga la COVID-19 umesababishja idadi ya watu wanaofanyia kazi nyumbani kuongezeka mara dufu na wafanyakazi hao wanahitaji ulinzi bora kwa sababu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mazingira duni.
Ripoti hiyo ya ILO, iliyopewa jina la “Kufanyia kazi nyumbani, kutojulikana hadi ajira zenye hadhi” inaeleza kuwa takriban watu milioni 260 walikuwa wanafanyia kazi nyumbani duniani kote wakiwakilisha asilimia 7.9 ya ajira zote duniani, na asilimia 56 kati yao au sawa na watu milioni 147 walikuwa wanawake.
Katika miezi ya kwanza ya janga la COVID-19 mwaka 2020, ripoti hiyo inakadiria kuwa mtu mmoja kati ya watano alijikuta analazimika kufanyia kazi nyumbani.
ILO katika ripoti hiyo iliyotolewa jana Januari 13, wafanyakazi hao wanajumuisha wale ambao wanafanyia kazi nyumbani wakati wote na idadi kubwa ya wafanyakazi ambao wanahusika katika kazi za uzalishaji bidhaa ambazo haiwezi kufanyika kwa mtandao kama vile ushonaji, kazi za sanaa na kuunda vifaa vya kielektroniki.
Kundi la tatu ni wafanyakazi wa majukwaa ya kidijitali ambao hutoa huduma kama vile kushughulikia madai ya bima, kuhariri nakala au kuchambua data kwa ajili ya mafunzo ya mifumo ya akili bandia (Artificial Inteligency).
“Kufuatia COVID-19, sasa idadi ya wanaofanyia kazi nyumbani imeongezeka mara dufu na wafanyakazi hao wanahitaji ulinzi bora kwani kufanyia kazi nyumbani huwa ni kwa faragha na mara nyingi wafanyakazi hawaonekani,” inaeleza ripoti hiyo.
Soma zaidi:
Ripoti imeongeza kuwa katika nchi za kipato cha chini na cha wastani, wafanyakazi wote wanaofanyia kazi nyumbani (asilimia 90) wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi.
Pia watu hao wanaofanyia kazi nyumbani hukabiliwa na hatari kubwa ya usalama na kiafya na wana fursa ndogo ya kupata mafunzo ikilinganishwa na wanaoenda maofisini, hali ambayo inaweza kuathiri matarajio na mafanikio ya ajira zao.
Mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo na afisa wa masuala ya uchumi wa ILO, Janine Berg amesema changamoto kubwa katika nchi nyingi ni kwamba kazi za kufanyia nyumbani hazina utaratibu maalum na sheria zilizopo haziwalindi kwani wengi huchukuliwa kama wafanyakazi binafsi na hivyo kutolewa kwenye kundi la sheria za ajira.
“Serikali, wafanyakazi na mashirika ya waajiri wanapaswa kushirikiana pamoja kuhakikisha kwamba watu wote wanaofanyia kazi nyumbani iwe wanashona vikapu Indonesia, wanatengeneza mafuta Ghana, wanasafisha picha Misri, wanashona barakoa Uruguay au wanafanyia kazi mtandaoni Ufaransa, wanapaswa kutoka na kuzigeuza kazi hizo zisizoonekana na kuwa ajira zenye hadhi,” amesema Berg.
Huenda idadi ya watu wanaofanyia kazi nyumbani ikaongezeka siku zijazo, jambo linalohitaji mikakati mathubuti ya kuwasaidia wafanyakazi kupata haki zao.