November 24, 2024

Corona yachangia kushuka bei ya mazao Tanzania

Amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo na bei ya mazao itaimarika.

  • Amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo na bei ya mazao itaimarika.
  • Awataka wakulima waendelee na kilimo katika kipindi hiki cha mpito. 
  • Amesema suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi, Serikali inasimamia tu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kushuka kwa bei ya mazao mbalimbali nchini Tanzania likiwemo zao la ufuta katika msimu wa mwaka huu kumechangiwa na janga la Corona na kuwataka wakulima waendelee na shughuli za kilimo kwani jambo hilo litakwisha. 

Amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo na bei ya mazao itaimarika baada ya kuongezeka kwa ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao nchini, ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa masoko na nchi itauza bidhaa zitokanazo na mazao hayo na si malighafi.

“Kushuka kwa bei ya ufuta kusiwakatishe tamaa na kuwafanya muache kulima kwa sababu bei haijashuka kwa zao hilo tu bali na mazao mengine kama chai, tumbaku, kahawa, chai na mazao mengine. 

“Hali hii imetokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambao umeikumba dunia,” amesema Waziri Mkuu jana Juni 24, 2020) wakati akizungumza na wananchi kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.


Zinahusiana: 


Majaliwa katika taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu amesema Serikali inatarajia kwamba kadiri ugonjwa wa COVID-19 unavyoendelea kupungua katika mataifa mbalimbali duniani hali ya bei ya mazao nayo itaimarika, hivyo wakulima waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho ni cha mpito.

“Suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi, Serikali inasimamia tu,” amesema Majaliwa.

Akiwa katika kata hiyo, Majaliwa amewaalika wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi waje kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali kwa sababu watakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi pamoja na nishati ya kutosha.