October 8, 2024

Corona yafuta mbio za mwenge wa uhuru Tanzania

Rais John Magufuli amesitisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2020 ikiwa ni tahadhari dhidi ya tishio la kusambaa kwa virusi vya Corona.

  • Rais Magufuli asitisha mbio hizo mpaka tatizo la virusi vya Corona litakapoondoka.
  • Awataka Watanzania kuchukua tahadhari kwa sababu ugonjwa huo unaua.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesitisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2020 ikiwa ni tahadhari dhidi ya tishio la kusambaa kwa virusi vya Corona. 

Virusi hivyo ambavyo vimetangazwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama janga la dunia umesababisha vifo vya zaidi ya watu 5,735 huku nchi za Italia na China zikiathirika zaidi.

Tayari nchi mbili za Afrika Mashariki za Rwanda na Kenya zimethibitisha kuwa na wagonjwa wa ugonjwa huo.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo asubuhi (Machi 16, 2020) wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu linalounganisha barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela, amesema ni lazima nchi ichukue tahadhari kwa sababu ugonjwa huo ni hatari na unaua.

Amesema amesitisha mbio za Mwenge kwa mwaka 2020 zilizotakiwa kuzinduliwa hivi karibu visiwani Zanzibar mpaka pale tatizo la ugonjwa wa virusi vya Corona utakapoisha.

“Ninafahamu kitu kingine kinacholeta mkusanyiko ni mwenge, tulitegemea kuwasha mwenge karibuni kule Zanzibar ambapo ungeweza kutembezwa nchi nzima, nimeamua mbio za mwenge hazitafanyika mpaka corona iwe imeondoka,” amesema Magufuli. 


Soma zaidi: 


Aidha, amesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya mbio za mwenge zitumike katika maandalizi ya kupambana na ugonjwa huo ikitokea umeingia nchini. 

“Ndugu zangu huu ugonjwa unaua, Watanzania tuchukue tahadhari, ugonjwa ushafika kwa majirani zetu (Rwanda na Kenya), ni lazima Watanzania tuchukue tahadhari utatumaliza,” amesema Magufuli.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli aliwataka Watanzania wanaosafiri ndani na nje ya nchi wasistishe safari zao na kuongeza kuwa Serikali itatoa vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa watendaji kama kuna sababu za msingi.

Baada ya kukagua ujenzi wa daraja la Ubungo, Rais Magufuli ameenda kukagua daraja la Kiyegeya mkoani Morogoro ambalo lilikatika na kuagiza mkoa ambao barabara itakatika meneja wa Tanroad mkoa atakuwa hana kazi.