July 5, 2024

Corona yakwamisha ujenzi mradi wa umeme wa Rusumo

Mradi huo wa megawati 80 ulianza kujengwa mwaka 2017 ulitakiwa kukamilika Februari mwaka huu

  • Wataalam waliokuwa wanajenga mradi huo waliondoka kukwepa janga la Corona.
  • Mradi huo wa megawati 80 ulianza kujengwa mwaka 2017 ulitakiwa kukamilika Februari mwaka huu. 
  • Sasa kukamilika 2021 baada ya wataalam kurudi. 

Dar es Salaam. Huenda wananchi wa nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu ili kufaidika na mradi wa kufua umeme wa Rusumo wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera kutokana na ujenzi wake kuathiriwa na janga la Corona. 

Mradi huo wa megawati 80 ulianza kujengwa mwaka 2017 ulitakiwa kukamilika Februari mwaka huu ukisimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi yenye wajumbe kutoka nchi hizo tatu.

Hata hivyo, mradi huo haujakamilika kama ilivyotarajiwa kwa sababu wataalamu wanaojenga mitambo ya kufua umeme huo waliondoka mapema mwaka huu kukwepa COVID-19.

“Ujenzi wa mradi huu ulianza mapema kabisa kwenye masuala ya usanifu na kwa mujibu wa mkataba mradi huu ulitakiwa kukabidhiwa mwezi Februari mwaka huu.

“Hali hiyo imeshindikana baada ya wataalam wa masuala ya umeme na ufungaji wa mitambo hiyo kuondoka kutokana na ugonjwa wa Corona ambao walikuwa wakitoka nchi za Ujerumani na India ambao wamekwama,” amesema Meneja mradi huo Mhandisi Patrick Lwesya jana (Septemba 14, 2020). 

Mhandisi Lwesya aliyekuwa akizungumza wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Alexander Kyaruzi kwenye mradi huo, amesema baada ya COVID-19 kushamiri nchi nyingi zilifunga mipaka yao na wataalamu waliokuwa wakihusika na ujenzi wa mradi huo upande wa umeme waliondoka na mpaka sasa kazi hiyo imesimama na kuzorotesha mradi.


Soma zaidi:


Hata hivyo, amesema ujenzi wa kuta na masuala mengine ya kuongozea maji na maeneo zitakapofungwa mashine (Pump house) unaosimamiwa na wakandarasi kutoka China ujenzi wake umefikia asilimia 74 kwa sababu wao wanaendelea na kazi.

Katika mradi huo, kila nchi itapata megawati 27 na kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme wa kilovoti 220 ambapo kwa upande wa Tanzania, miundombinu hiyo  itaingiza umeme katika gridi ya Taifa kupitia njia  ya umeme inayotoka mkoani Geita na  vijiji  13 vinavyopitiwa na mradi wa Rusumo vitasambaziwa nishati hiyo. 

Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco, Alexander Kyaruzi amesema yeye pamoja wakurugenzi hawajafurahia  kasi ya ujenzi huo kutokana na mradi kuchelewa na kusababisha malengo yaliyowekwa kukwama.

Amesema wataalam wameanza kurudi na wataendelea na kazi ambapo mradi huo utakamilika Desemba 2021.

Mradi wa kufua umeme Rusumo unajengwa kwa mkopo wa Dola za Marekani milioni 340 (Sh788.6 bilioni) kutoka Benki ya Dunia.