Corona yasababisha wafanyakazi 900 kuondolewa kazini
Kampuni hiyo ambayo inafanya kazi mtandaoni imekuwa ikiwasaidia watu wanaosafiri kupata hoteli na maeneo ya utalii duniani.
- Ni kampuni ya Trip Advisor ya Marekani imefuta kazi wafanyakazi hao duniani kupunguza gharama za uendeshaji.
- Sambamba na watu hao kukosa ajira, kampuni hiyo imefunga ofisi mbili kukwepa makali ya corona.
- Maamuzi ya Trip Advisor ni mwendelezo wa makali ya Corona yanayozikumba kampuni nyingi ulimwenguni.
Dar es Salaam. Kampuni ya ushauri wa safari ya Trip Advisor ya Marekani imewafuta kazi wafanyakazi wake 900 ulimwenguni ili kupunguza gharama za uendeshaji baada ya ugonjwa wa Corona unaosumbua dunia kuathiri shughuli za utalii na usafiri ambazo kampuni hiyo inazitegemea kupata mapato.
Kampuni hiyo ambayo inafanya kazi mtandaoni imekuwa ikiwasaidia watu wanaosafiri kupata hoteli na maeneo ya utalii duniani.
Idadi hiyo ya wafanyakazi waliopoteza ajira ni sawa na asilimia 25 ya wafanyakazi wake wote ambapo kati yao, 600 ni wa nchini Marekani huku waliobaki wapo katika ofisi zake zilizopo katika nchi mbalimbali duniani.
Zinazohusiana
- Corona kuhatarisha ajira bilioni 1.6 duniani
- Shirika la ndege la Afrika Kusini kufungwa, wafanyakazi 4,700 kupoteza ajira
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo iliyoripotiwa na shirika la habari la Gulf News, kampuni hiyo pia imefunga ofisi za San Francisco na Downtown Boston za Marekani ikiwa ni njia ya kupunguza gharama.
Hata hivyo, kwa wafanyakazi ambao wanabaki kwenye kampuni hiyo watalazimika kupokea pungufu ya asilimia 20 tu ya mshahara wao.
Athari za ugonjwa wa virusi vya Corona zimeendelea kujidhihirisha katika maeneo mbalimbali dunia hasa katika sekta za utalii, usafiri ambazo zimekuwa zikitegemewa na watu wengi kujipatia kipato.