October 6, 2024

Corona yasababisha watu kutazama filamu vibarazani Hispania

Katika jiji la Madrid nchini Hispania, watu wanatazama filamu kutoka kwenye vibaraza vya nyumba zao baada ya Serikali kuwawekea skrini kubwa mitaani ili kuwaleta watu pamoja na kuwaondolea upweke.

Watu wakiwa kwenye nyumba zao wakitazama filamu zilizowekwa kwenye skrini kubwa nje. Picha| Mtandao.


  • Watu wanatazama filamu kutoka kwenye vibaraza vya nyumba zao baada ya Serikali kuwawekea skrini kubwa mitaani ili kuwaleta watu pamoja.
  • Skrini hiyo ambayo iko juu ya gari huzunguka kila siku jioni katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo.
  • Hiyo inawasaidia wako pamoja na wapendwa wao.

Licha ya nchi nyingi duniani kuwazuia kutoka nje ikiwa ni tahadhari ya kuwakinga na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, wabunifu wanaendelea kutafuta suluhisho la kuwafanya wawe na furaha wakiwa nyumbani. 

Katika jiji la Madrid nchini Hispania, watu wanatazama filamu kutoka kwenye vibaraza vya nyumba zao baada ya Serikali kuwawekea skrini kubwa mitaani ili kuwaleta watu pamoja.

Skrini hiyo ambayo iko juu ya gari huzunguka kila siku jioni katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo, ili watu waangalie filamu na majirani zao huku kila mtu akiwa nyumbani kwake. 

Naibu Meya wa jiji hilo, Begona Villacis ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa lengo sinema na filamu hizo kuonyeshwa mitaani ni kuwafanya watu hasa waliozoe kwenda kwenye kumbi za sinema waendelee kufurahia hata wakiwa nyumbani. 

Amesema baadhi ya watu waliwasilisha maombi yao kuhusu kuonyeshwa kwa filamu katika mitaa ikizingatiwa kuwa ni wiki ya sita sasa tangu wananchi wa jiji hilo wazuiliwe kutoka nje ili kujikinga na COVID-19. 


Zinazohusiana


BBC imeeleza kuwa baadhi ya watu wanajisikia wapweke kukaa ndani, hivyo wanahitaji kurudi katika maisha ya kawaida na njia mojawapo ni kuangalia filamu katika vibaraza vya nyumba zao.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hadi Mei 1, 2020 zinaeleza kuwa watu 213, 435 wa nchi hiyo wameambukizwa ugonjwa huo huku 24,543 wakifariki dunia. 

Skrini hizo huwa juu ya gari na hutembezwa katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo ili watu watazame filamu. Picha|Mtandao.